Dar es Salaam. Mara zote ubunifu hufanyika pale ambapo unataka kurahisisha ufanyaji wa kazi fulani, wakati mwingine bila kujua hatua hii inaweza kusaidia maelfu ya watu na kuboresha huduma za jamii.

Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Dk Niek Versteegde, Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi mwenza wa GOAL 3, alivyojikuta akifanya majukumu ya kazi kuwa rahisi kwa watumishi wa afya wakati akijaribu kutatua changamoto ya huduma za dharura katika Hospitali ya Sengerema.

GOAL 3 ni shirika la kiteknolojia la afya lenye makao yake nchini Uholanzi na Rwanda, linalolenga kuboresha huduma za afya katika nchi zinazoendelea kupitia teknolojia bunifu.

Mradi wake mkuu wa majaribio, unaojulikana kama IMPALA system, unalenga kupunguza vifo vya watoto na wajawazito kwa kutumia mashine za kisasa za kufuatilia hali ya mgonjwa, zilizounganishwa na programu ya kompyuta (software) ili kusaidia madaktari kufanya maamuzi ya haraka.

Dk Niek amesema uamauzi huo ulilenga kusaidia utoaji wa huduma za haraka kwa watoto baada ya kubaini kuwa hata baada ya kuanzisha kitengo cha huduma za watoto wachanga katika hospitali hiyo, bado kulikuwa na mapungufu kutokana na uhaba wa watumishi na vifaa.

Hali hii ilisababisha wahudumu wa afya, kulazimika kuingia katika mzunguko unaochosha wakati wa kutoa huduma za dharura.

“Nilikuwa nikikimbia kutoka tukio moja la dharura moja hadi lingine, mara nyingi nikiingilia kwa kuchelewa na kufanya matibabu kukosa ufanisi au kuchukua muda mrefu na kuongeza gharama. Ni kama kupambana na moto bila kuwa na uwezo wa kuuzuia,” amesema.

Amesema kupitia uzoefu huo kampuni yake ililazimika kutengeneza suluhisho litakalowawezesha wahudumu wa afya kufuatilia na kusimamia wagonjwa wao kwa ufanisi zaidi katika mazingira ya namna hiyo.

“Lengo ni kuvunja huo mzunguko, kuboresha matokeo ya afya kwa watoto, kuongeza ubora wa huduma na kupunguza mzigo wa kazi pamoja na gharama,” amesema.

Kupitia ubunifu huo sasa watoto wachanga wanaozaliwa wanakuwa na uwezo mkubwa wa kuishi, kwani mfumo uliowekwa unakuwa na uwezo wa kusoma kile kinachotakiwa kufanyika kwa wakati husika.

Katika hatua za majaribio ili kupima ufanisi wa mfumo huo, kwa jiji la Dar es Salaam majaribio yalifanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Amana, Mwananyamala, Temeke Pamoja na hospitali za wilaya ambapo kwa Temeke ilikuwa Yombo ya Vituka na Kinondoni ikiwa Hospitali ya Mwambwepande na Kivule kwa Ilala.

“Tunaona kupungua kwa vifo vya watoto wachanga na watoto kwa kiwango kikubwa kwa kati ya asilimia 20 hadi 50. Pia tunaona kupungua kwa mzigo wa kazi kwa wahudumu wa afya,” amesema.

Vifaa hivyo vina uwezo wa kutoa taarifa za kila mtoto katika ‘monitor’ moja inayoangaliwa na muuguzi, jambo ambalo linaweka urahisi wa kutoa huduma inayotakiwa kwani ikiwa kuna hali ya hatari hupiga kelele za tahadhari na kumwambia muuguzi mtoto aliye kitanda namba ngapi anahitaji huduma gani.

Akizungumzia suala hilo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Dk Jonas Lulandala amesema mradi huo umekuwa ukiendeshwa kwa kutumia fedha za Serikali lakini pia na michango mikubwa ya wadau wakiwepo ni IHI 360.

“Lengo ni kwa ajili ya kuokoa maisha ya watoto wachanga ambao wamekuwa wakipoteza maisha katika hatua za awali, ikiwemo kuwa na uzito pungufu na hivyo kushindwa kutambuliwa kwa usahihi na kupata matibabu sahihi, kuzaliwa akapata sukari ya kushuka, kuwa na joto la juu lakini akashindwa kutambuliwa na kupewa matibabu,” amesema.

Vifaa hivyo vinawezesha kutambua changamoto mtoto anayokuwa nayo anapofungiwa kifaa hicho kutoa taarifa sahihi juu ya nini kinahitajika kufanyika.

Amesema vifaa hivyo vinatoa taarifa kwa muuguzi pale anapokuwa amekaa badala ya kumtembelea mmoja mmoja, ataambiwa ni mtoto yupi na tatizo lake ni lipi.

“Ile monitor itamwambia inabidi amwangalie mtoto gani ana shida gani, kama ni sukari iko chini inasema  ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa,” amesema.

Hata hivyo, Rais wa Chama Cha Madaktari wa watoto nchini Tanzania, Dk Theopista Masege amesema licha ya vifo vya watoto wachanga kupungua lakini bado jitihada zaidi zinatakiwa kufanyika.

“Kwa wastani wanazaliwa watoto milioni 2.5 na kati yao kila watoto 24 kwenye watoto 1,000 wanafariki. Ukiweka katika namba halisi ni sawa na watoto 55,000 kwa mwaka, ambao ni sawa na watoto 150 kila siku, hivyo unaweza kuona bado tuna kazi kubwa ya kufanya,” amesema.

Amesema ni vyema kuhakikisha kuwa kila mtoto anaishi na anapata nafasi ya kutimiza ndoto zake ikiwemo kuwa kiongozi wa kesho kwa kufikisha njia zinazoonekana kuleta matunda katika kila hospitali na kituo cha afya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *