Dodoma. Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba Tanzania (TMDA) imetoa msaada wa dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya Sh16.9 milioni kwenye Gereza Kuu la Isanga lililopo jijini Dodoma.

Dawa na vifaatiba hivyo ni vile vilivyokamatwa katika maduka ya dawa wakati wa ukaguzi unaofanywa na mamlaka hiyo, baada ya kubainika kuwa havistahili kuwepo katika maeneo hayo, ikiwemo dawa zenye nguvu kubwa na zile zenye asili ya kulevya.

Akizungumza leo, Alhamisi, Aprili 2, 2026, jijini Dodoma wakati wa kukabidhi msaada huo, Meneja wa TMDA Kanda ya Kati, Sonia Mkumbwa, amesema mamlaka hiyo haina hospitali ya kupeleka dawa na vifaa tiba hivyo, hivyo huvipeleka kwenye taasisi za umma zinazotoa huduma kwa jamii.

“Bidhaa hizi tumezitoa kwenye soko, ambapo huwa tunafanya ukaguzi katika maeneo yanayouza, kuhifadhi na kusambaza bidhaa za dawa na vifaa tiba.

“Kutokana na kanuni za makundi ya dawa, kuna maeneo yenye wigo maalumu wa dawa wanazoruhusiwa kuhifadhi. Tunapobaini ukiukwaji, tunaziondoa,” amesema Mkumbwa.

Meneja wa Mamlaka ya dawa na vifaa tiba Tanzania (TMDA), Kanda ya kati Sonia Mkumbwa (wa tatu kushoto) akimkabidhi boksi la dawa Mkuu wa gereza kuu la Isanga, Wiliam Makwaya leo Aprili 2, 2026. Wengine ni maofisa kutoka magereza na TMDA Kanda ya kati.

Ameongeza kuwa, wakati mwingine dawa zinazokutwa katika maduka hayo ni zenye nguvu kubwa au zenye asili ya kulevya, ambazo haziruhusiwi kuhifadhiwa katika maduka ya dawa muhimu kutokana na kukosa wataalamu na mazingira stahiki.

Mkumbwa amesema TMDA haina hospitali wala zahanati, hivyo dawa zinazoondolewa sokoni hutolewa kama msaada kwenye taasisi za umma zenye uhitaji, hususan magereza ambako kuna mahitaji makubwa ya huduma za afya.

“Tunapopata dawa hizi, tunazirudisha kwa jamii kupitia taasisi hizi ili ziwasaidie wahitaji, wakiwemo wanafunzi wanaorekebishwa tabia (wafungwa), maofisa wanaofanya kazi katika maeneo hayo pamoja na jamii inayowazunguka,” amesema.

Amesema msaada huo unalenga kupunguza upungufu wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya vinavyosimamiwa na magereza, ambavyo wakati mwingine vinashindwa kukidhi mahitaji kwa asilimia 100.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Gereza Kuu Isanga, Dk Pantaleo Maumba, amesema TMDA imekuwa msaada mkubwa kwao kila mwaka, hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa magonjwa yanayochangiwa na mvua na upepo, ikiwemo mafua makali.

“Kweli mnatuokoa sana kwa sababu kila mwaka tunapata huduma yenu. Sisi tupo mstari wa mbele kupambana na magonjwa ana kwa ana, hivyo vifaa na dawa hizi zinaturahisishia kazi,” amesema Dk Maumba.

Naye Mkuu wa Gereza Kuu Isanga, William Makwaya, ameshukuru kwa msaada huo, akisema utasaidia kuboresha huduma za afya kwa wafungwa pamoja na jamii inayozunguka gereza hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *