Iringa. Kupanda kwa bei ya mafuta kulikotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) na kuanza kutekelezwa mapema Aprili mwaka huu, kumeibua taharuki katika sekta ya usafiri wa umma ndani ya Manispaa ya Iringa.
Hali hiyo imewalazimu baadhi ya madereva wa vyombo vya usafiri kupandisha nauli ili kukabiliana na ongezeko la gharama za uendeshaji, huku abiria wakilalamikia mzigo mpya wa maisha unaotokana na hatua hiyo.
Uchunguzi wa Mwananchi Digital uliofanyika Aprili 3, 2026 umebaini kuwa baadhi ya madereva, hususan wa bajaji, tayari wameanza kuongeza nauli kutoka Sh800 hadi Sh1,000 kwa safari za ndani ya mji.
Madereva hao wanasema hawakuwa na chaguo jingine kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta, jambo linalopunguza mapato yao na kuongeza gharama za uendeshaji wa kila siku.
“Hali imekuwa ngumu sana, mafuta yamepanda na hatuwezi kuendesha kwa hasara. Ndiyo maana tumelazimika kuongeza nauli, ingawa tuna hofu ya kupoteza wateja,” alisema dereva wa bajaji, Juma Kalindu.
Dereva mwingine, Rashid, amesema ongezeko hilo limepunguza idadi ya wateja, lakini akasisitiza kuwa ni hatua ya lazima ili kuendelea na shughuli zao.
Kwa upande wa madereva wa daladala, wengi wao bado hawajafanya mabadiliko ya nauli wakisubiri mwongozo rasmi kutoka serikalini ili kuepuka migogoro na abiria.
Baadhi ya abiria wakilipa nauli baada ya safari yao kutoka Ipogolo mpaka stendi ya bajaji Miyomboni Manispaa ya Iringa. Picha na Christina Thobias
“Bado hatujapandisha nauli kwa sababu tunasubiri mwongozo wa Serikali. Hatutaki kuingia kwenye migogoro na abiria, lakini gharama za mafuta zimekuwa kubwa,” alisema dereva wa daladala, Mussa Gambo.
Naye Selemani Ndazi amesema kupandisha nauli bila utaratibu kunaweza kusababisha mvutano, hivyo kuna haja ya mamlaka husika kutoa viwango rasmi.
Kwa upande wa abiria, wengi wameeleza kuwa ongezeko la nauli limeathiri kwa kiasi kikubwa maisha yao ya kila siku, wakidai kuwa hali hiyo imeongeza gharama za maisha huku kipato kikiendelea kubaki kilekile.
Mkazi wa Iringa mjini, Neema Tweve, amesema wamelazimika kupunguza safari zisizo za lazima kutokana na nauli kuwa juu.
“Kipato ni kilekile lakini gharama zimeongezeka. Tunabana matumizi na baadhi ya safari tunaziacha kabisa,” alisema.
Paulo Kyando, mfanyakazi wa sekta binafsi, amesema nauli imeanza kuchukua sehemu kubwa ya kipato chake, jambo linaloathiri mahitaji mengine muhimu.
Naye Rehema Mbuma amesema wakati mwingine hulazimika kutembea umbali mrefu ili kuokoa nauli, hali inayoonyesha uzito wa changamoto hiyo kwa wananchi wa kawaida.
Athari hizo pia zimeanza kuonekana katika shughuli za biashara, ambapo mfanyabiashara John Minja amesema ongezeko la gharama za usafiri limepunguza uwezo wa wateja kununua bidhaa.
Katika maeneo ya pembezoni, hali ni ngumu zaidi kwa watumiaji wa bodaboda, hasa wanaotegemea usafiri huo kufika mashambani na kusafirisha mazao.
Dereva wa bodaboda katika eneo la Tumaini, Shabani Balama, amesema gharama za mafuta zimepanda huku abiria wengi wakishindwa kumudu nauli mpya.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, bei ya mafuta katika Manispaa ya Iringa imepanda kutoka Sh2,877 hadi Sh3,920 kwa lita, hali inayoongeza presha kwa wadau wa usafiri na watumiaji wa huduma hizo.
Kutokana na hali hiyo, wananchi wameiomba Serikali kupitia mamlaka husika kuweka viwango rasmi vya nauli vitakavyolinda maslahi ya madereva na abiria, ili kuhakikisha huduma za usafiri zinaendelea kwa utulivu na kuepusha migogoro.