Simiyu. Wananchi wa Mkoa wa Simiyu wamesema kuwa usimamizi mzuri wa ardhi na upangaji wa matumizi yake ni muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa makazi bora na yenye mpangilio kwa jamii.

Wakizungumza leo Aprili 3, 2026, wamesema kuwa changamoto za migogoro ya ardhi, ujenzi holela na ukosefu wa mipango bora ya matumizi ya ardhi zimekuwa zikikwamisha juhudi za wananchi wengi kujenga makazi bora na salama.

Mkazi wa Nyakabindi wilayani Bariadi, Paulo Ngeleja amesema kukosekana kwa mipango madhubuti ya matumizi ya ardhi katika baadhi ya maeneo kunasababisha wananchi kujenga nyumba bila mpangilio.

“Watu wengi wanajenga nyumba mahali wanapopata tu bila mpango maalumu. Hii inasababisha wakati mwingine kukosekana kwa barabara na huduma muhimu kama maji na umeme,” amesema.

Kwa upande wake, Rehema Alfa, mkazi wa Maswa amesema migogoro ya ardhi nayo imekuwa kikwazo kwa wananchi kuendeleza maeneo yao.

“Unakuta mtu anaogopa kuendeleza eneo lake kwa sababu kuna migogoro ya mipaka au umiliki wa ardhi. Kama ardhi itasimamiwa vizuri, wananchi wataweza kujenga makazi bora,” amesema Rehema.

Naye John Ntugwa, mkazi wa wilaya ya Meatu, amesema elimu kuhusu matumizi sahihi ya ardhi inahitajika zaidi kwa wananchi ili kuepuka ujenzi holela.

Picha ikionesha sehemu ya mji wa Bariadi ambao ndiyo makao makuu ya mkoa wa Simiyu. Picha na Maktaba

“Watu wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu mipango ya matumizi ya ardhi. Serikali ikitoa elimu zaidi, itasaidia kupanga makazi vizuri,” amesema Ntugwa.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, amesema serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha usimamizi wa ardhi ili kuhakikisha makazi ya wananchi yanakuwa bora na yenye mpangilio.

“Usimamizi mzuri wa ardhi ni msingi wa maendeleo ya makazi na miji yetu. Tunasisitiza wananchi kufuata taratibu za upangaji wa maeneo na kupata hati au nyaraka halali za umiliki wa ardhi,” amesema Macha.

Amesema serikali itaendelea kushirikiana na halmashauri za wilaya kuhakikisha mipango ya matumizi ya ardhi inatekelezwa ipasavyo ili kupunguza migogoro na kuboresha makazi ya wananchi.

Macha amewataka pia wananchi kuepuka ujenzi holela na kufuata taratibu za ujenzi ili kuwezesha upatikanaji wa huduma muhimu kama barabara, maji na umeme katika maeneo yao ya makazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *