Tanga. Hofu ya milipuko ya magonjwa imewakumba zaidi ya wafanyabiashara 1,500 katika Soko la Mgandini jijini Tanga, kufuatia uchafu uliokithiri na ukosefu wa vyoo katika eneo hilo linalotegemewa na wananchi wengi kwa biashara ya mbogamboga na matunda.
Wafanyabiashara hao wamesema licha ya malalamiko yao ya muda mrefu kwa Halmashauri ya Jiji la Tanga, hali ya usafi katika soko hilo imeendelea kuwa mbaya, huku dampo la taka likifurika katikati ya soko na kuacha harufu kali inayowakera wafanyabiashara na wateja.
Asubuhi ya Ijumaa, Aprili 3, Mwananchi imetembelea soko hilo kushuhudia dampo likiwa limejaa taka kupita kiasi huku vyoo vilivyopo vikiwa vimefungwa kwa kufuli kutokana na chemba zake kujaa, hali inayowalazimu wafanyabiashara kutafuta njia mbadala za kujisaidia.
Dampo lililofurika uchafu lililopo kwenye soko kuu la mbogamboga na matunda la Mgandini linalolalamikiwa kwa kutoa farufu kali na kusababisha kero kwa wananchi na wafanyabiashara wanaotumia soko hilo.Picha na Mbonea Herman
Baadhi yao wamesema wakati wa mvua hali inakuwa mbaya zaidi kwani maji husomba uchafu na kuuelekeza kwenye maeneo ya biashara na hata kwenye bidhaa wanazouza.
Mfanyabiashara wa mbogamboga katika soko hilo, Alfani Ismaili, alisema hali ya soko hilo imekuwa hatari kwa muda mrefu kutokana na taka kukusanywa katikati ya soko bila kuondolewa kwa wakati.
“Soko lote hili halina choo kinachofanya kazi. Wafanyabiashara wa kiume tunalazimika kujisaidia kwenye mfereji, na maji yanayotiririka yanakuja hadi hapa tunapouzia bidhaa. Hali hii inaweza kusababisha magonjwa makubwa,” amesema Ismaili.
Mfanyabiashara mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Kidevu amesema dampo hilo limefikia hatua ya kuzuia hata magari yanayoleta bidhaa sokoni kupita.
“Magari yanakuja kuleta nyanya lakini yanashindwa kupita kwa sababu dampo limeziba njia. Harufu ni kali sana na wateja wengine wanakimbia. Tunaishi kwa hofu ya magonjwa kama kipindupindu,” amesema Kidevu.
Katibu wa Soko la Mgandini, Shaban Shaban, amesema uongozi wa soko umekuwa ukilalamikia hali hiyo kwa muda mrefu bila mafanikio.
“Kwa kweli hali ya hapa inatisha. Kuna haja ya halmashauri kuhakikisha taka hazikai hapa kwa muda mrefu. Wakati Rais Samia Suluhu Hassan alipokuja Tanga, kulikuwa hakuna taka kabisa, lakini baada ya kuondoka hali imebadilika,” amesema Shaban.
Katika hatua nyingine, Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga kimeonyesha kukerwa na hali hiyo na kuitaka halmashauri kuchukua hatua za haraka.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdallah, ametoa wiki moja kwa Halmashauri ya Jiji la Tanga kuhakikisha usafi wa soko hilo unarejeshwa na changamoto ya vyoo inapatiwa ufumbuzi.
“Hatuwezi kuvumilia uzembe unaowaathiri wananchi wanaotegemea soko hili kwa kipato chao. Ni lazima hatua zichukuliwe mara moja,” amesema Abdallah.
Akijibu malalamiko hayo, Meya wa Jiji la Tanga, Mustapha Seleboss, amesema jiji linaendelea na jitihada za kuboresha miundombinu ya soko hilo, ikiwemo ujenzi wa barabara za ndani pamoja na mpango wa kujenga choo kipya kwa gharama ya Sh milioni 32.
Hata hivyo, wafanyabiashara wanasema wanahitaji hatua za haraka zaidi, wakisisitiza kuwa afya zao na za wateja iko hatarini.
“Tunapata shida sana, wakati mwingine tunalazimika kwenda mbali kujisaidia. Hii si hali inayopaswa kuwepo katika soko la jiji,” amesema mfanyabiashara Salma Ramadhan.