Moroni. Serikali ya Umoja wa Visiwa vya Comoro imemtunuku aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini humo, Said Yakub, nishani ya Mwezi wa Kijani (Order of the Green Crescent) kutambua mchango wake katika kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kijamii kati ya mataifa hayo mawili jirani.
Nishani hiyo yenye heshima kubwa ilikabidhiwa rasmi na Rais wa Comoro, Azali Assoumani, katika hafla iliyofanyika jijini Moroni na kuhudhuriwa na viongozi waandamizi wa Serikali, mawaziri, viongozi wa dini, na wadau wa sekta binafsi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Rais Assoumani amempongeza Yakub kwa utumishi uliotukuka na kujituma kwake binafsi katika kuendeleza uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Comoro.
Amemtaja kuwa balozi aliyefanya kazi kwa ubunifu na matokeo yanayoonekana.
“Hapa duniani kuna vitu viwili ambavyo mtu hawezi kuchagua: jirani yako na ndugu yako. Comoro na Tanzania ni majirani na pia ni ndugu, hivyo uhusiano wetu ni wa lazima na wa kudumu,” amesema.
Ameeleza huku akimtaka Yakub kuendelea kuwa balozi mwema wa Comoro popote atakapokuwa.
Balozi Yakub aliteuliwa kushika wadhifa huo Aprili 2024, na tuzo hiyo imekuja ikiwa ni sehemu ya kumuaga baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa.
Katika hafla hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro, Mohamed Mbae, ameeleza kuwa Yakub atakumbukwa kwa mchango wake katika kufanikisha Kamisheni ya Kudumu ya Pamoja (JPC), ambayo imekuwa msingi wa mafanikio ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo.
Mbali na diplomasia, Yakub pia ameacha alama katika sekta ya afya. Kupitia uratibu wake, madaktari bingwa kutoka Tanzania walitoa huduma za kibingwa kwa zaidi ya wananchi 6,000 wa Comoro ndani ya miaka miwili, idadi inayokaribia wagonjwa wanaohudumiwa na hospitali kuu ya taifa hilo kwa mwaka mzima.
Amesema jitihada hizo zimechochea pia ukuaji wa utalii wa matibabu; kwa sasa wananchi wa Comoro wanaosafiri kwenda Tanzania kwa matibabu wanachangia Sh240 bilioni katika uchumi.
Kwa upande wa biashara, takwimu za Wizara ya Viwanda na Biashara Tanzania zinaonyesha kuwa thamani ya biashara kati ya nchi hizo imeongezeka ndani ya kipindi cha miaka miwili kutoka Sh90 bilioni hadi kufikia Sh180 bilioni.
Akitoa salamu za shukurani, Yakub amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano imara kati ya viongozi wa mataifa hayo mawili.
“Namshukuru sana Rais wangu kwa kuniamini kunituma Comoro na sasa Ufaransa. Mafanikio yote yaliyopatikana hapa yametokana na maelekezo yake na uhusiano mzuri na mwenzake wa hapa,” amesema Yakub.
Nishani ya Order of the Green Crescent hutolewa kwa watu waliotoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya Comoro. Miongoni mwa waliowahi kuitunukiwa ni pamoja na aliyekuwa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Akinwumi Adesina.