
Marekani na Qatar, zimeitisha raundi mpya ya mazungumzo kati ya waasi wa M23 na Serikali ya DRC, mazungumzo yaliyopangwa kufanyika katikati ya mwezi huu huko Uswis, hii ni kwa mujibu wa kituo cha utafiti nchini Congo, CRG.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Awali mazungumzo haya yalikuwa yamepangwa kufanyika mjini Doha, lakini yamehamishwa kutokana na mzozo unaoendelea kwenye nchi za Ghuba.
Mazungumzo haya yanaenda kufanyika huku licha ya kusitishwa mapigano baina ya pande hizo kufuatia makubaliano ya Doha ya Novemba 15 na kisha yale ya Washington mwezi Desemba, hatua kidogo tu ndizo zimepigwa.
Kati ya masuala nane yaliyojadiliwa, ni mambo mawili tu ndio yalikubaliwa, mpango wa kufuatilia usitishaji mapigano na kubadilishana wafungwa wa kivita.
Suala la mustakabali wa M23, kurejea kwa wakimbizi na Kutenda haki kwa makosa ya kivita yaliyotekelezwa na pande zote, yamesalia magumu Kinshasa na waasi hao wakitofautiana.
Katika mzozo huu, Rwanda inatajwa moja kwa moja kuwasaidia waasi hao, ambapo mwezi uliopita Marekani ilitangaza vikwazo kwa maofisa wa juu wa jeshi la Rwanda, Washington ikiituhumu Kigali kukiuka kwa makusudi makubalino waliyotiliana Saini na Kinshasa.
Wakati Serikali ikitaka waasi hao kuachia miji wanayokalia, M23 kwa upande wake inataka marekebisho ya Katiba yatakayotambua mamlaka yake na kutoa uhuru wa kujiongoza kwa majimbo ya Kivu.