
KWA miaka mingi, Tanzania imekuwa uwanjani, lakini si kwenye mbio za fedha kubwa za riadha duniani.
Zaidi ya yote, imekuwa nyuma hata katika kujenga mwendelezo wa uwakilishi wa wanariadha wa masafa marefu kwenye majukwaa makubwa.
Wakati mataifa jirani yakivuna mamilioni kupitia mashindano ya kimataifa, udhamini na mikataba ya matangazo, Tanzania imeendelea kubaki nyuma, ikishindwa kunufaika ipasavyo na uchumi wa riadha.
TATIZO LINA MIZIZI MUDA MREFU
Baada ya enzi za dhahabu za mwanariadha kama Filbert Bayi, Tanzania ilishindwa kuendeleza mafanikio hayo kwa mfumo thabiti. Badala yake, iliendelea kutegemea vipaji na bidii ya mtu mmoja mmoja bila kujenga misingi ya kudumu.
Matokeo yake ni pengo kubwa la muda kati ya nyota mmoja na mwingine, hadi kuibuka kwa Alphonce Simbu baada ya miongo kadhaa.
Ukosefu huu wa mfumo umeigharimu nchi si kwa medali tu, bali pia kwa fedha nyingi. Leo, riadha si mchezo wa kukimbia tu, ni biashara kubwa inayozungusha mamilioni ya dola.
Kwa mujibu wa watalamu, washindi wa mbio kubwa duniani kama London, Berlin na Chicago Marathon hulipwa kati ya Dola 55,000 hadi 100,000, huku bonasi zikisukuma mapato hadi zaidi ya Dola 150,000.
Hata wale wasiopanda jukwaani hupata fedha kupitia ada za ushiriki (appearance fees), udhamini na matangazo, wakati mwingine hadi Dola 100,000 kwa mbio moja.
Wataalamu wa michezo wanasema, kwa msimu mmoja tu, mwanariadha wa kiwango cha juu anaweza kuvuna zaidi ya Dola 300,000. Hata hivyo, Tanzania haijaonekana mara kwa mara kwenye jukwaa hili la fedha kubwa.
VIPAJI VIPO, MFUMO HAKUNA
Hakuna ubishi kuwa Tanzania imebarikiwa vipaji vya riadha. Lakini vipaji hivyo havijageuzwa kuwa mafanikio ya kudumu.
Mwanariadha nyota wa taifa, Alphonce Simbu, ameonyesha kuwa inawezekana kushindana na wakubwa duniani. Hata hivyo, mafanikio yake yamechangiwa zaidi na jitihada binafsi kuliko mfumo wa kitaifa.
“Vipaji vipo, lakini msaada ni mdogo,” amewahi kusema Simbu.
Kauli hii inaeleza kwa ufupi changamoto iliyopo- ukosefu wa mfumo endelevu wa kukuza vipaji.
Mtaalamu wa michezo, Dk Hemed Suleiman, anasema Tanzania inapoteza mamilioni ya fedha kila mwaka kutokana na hali hiyo.
“Tunakosa mamilioni kwa sababu hatuna mfumo wa kukuza vipaji na kuvifikisha kwenye soko la kimataifa,” anaiambia Mwanaspoti.
Anaongeza kuwa, “tumekuwa tukitegemea juhudi za mtu mmoja mmoja badala ya kujenga mfumo. Hii ina maana tunapoteza si tu medali, bali pia fedha nyingi ambazo wanariadha wetu wangeweza kuingiza kila mwaka.”
Kwa mfano, anasema, kama Tanzania ingekuwa na wanariadha watano tu wa kiwango cha juu wanaoshiriki mashindano makubwa kila mwaka, kila mmoja akipata wastani wa dola 80,000, taifa lingeingiza angalau dola 400,000 moja kwa moja.
Ukijumlisha udhamini, matangazo, kambi za mazoezi na utalii wa michezo, mapato hayo yangepanda hadi mamilioni ya dola.
Lakini fedha hizo zimeendelea kuwanufaisha wengine.
Kwa nchi zilizo na mifumo imara, mapato haya huleta faida pana zaidi, kuanzia fedha za kigeni hadi ajira katika ukocha, sayansi ya michezo, usimamizi wa wanariadha na huduma nyingine.
SIRI YA MAJIRANI KWENYE RIADHA
Wakati Tanzania ikisuasua, majirani walishtuka mapema. Uganda imewekeza kwa makusudi katika mfumo wa kukuza riadha, kuanzia mafunzo ya miinuko (high altitude), maandalizi ya kitaalamu hadi usimamizi wa wanariadha.
Matokeo yake yanaonekana wazi. Wanariadha kama Joshua Cheptegei na Jacob Kiplimo sasa ni mabingwa wa dunia na wanavuna fedha kubwa katika mashindano ya kimataifa.
Mchambuzi wa michezo, Moses Kato, anasema siri yao ni mtazamo.
“Uganda waliwekeza kwenye mfumo na wakaichukulia riadha kama sekta ya kiuchumi, si mchezo tu,” anasema.
Kwa upande mwingine, Kenya bado ni mfano wa kuigwa.
Wamejenga mfumo kamili unaounganisha utamaduni, jiografia na taasisi. Riadha kwao si burudani, ni ajira na chanzo cha kipato. Maelfu ya vijana wanaishi kupitia mchezo huo.
Katika mazingira haya, mafanikio ya Simbu yanaendelea kuonyesha kuwa Tanzania ina uwezo mkubwa ambao bado haujatumiwa ipasavyo. Hata hivyo sasa kuna matumaini.
Baada ya miaka ya kupoteza fursa, sasa kuna dalili za mabadiliko.
Katika Kili Marathon 2026, hivi karibuni Waziri wa Michezo, Paul Makonda alitangaza mpango wa kuanzisha vituo maalum vya mazoezi katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Lengo ni kujenga mfumo wa kuibua, kukuza na kuandaa wanariadha kwa ushindani wa kimataifa. Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa miundombinu pekee haitoshi.
“Tunahitaji makocha bora, sayansi ya michezo, lishe sahihi na usimamizi wa wanariadha,” anasisitiza Kato.
Kwa upande mwingine, Tanzania ina hazina kubwa ya vijana, zaidi ya asilimia 75 wakiwa chini ya miaka 35.
Hii ni nguvu kazi inayoweza kuigeuza nchi kuwa kitovu cha riadha duniani ikiwa itapewa mwelekeo sahihi, kuanzia ngazi za chini (shuleni).