
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa vitisho vya Marekani vya kushambulia miundombinu ya nishati ya Iran ni kukiri wazi nia ya kutenda uhalifu wa kivita.
Sayyid Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayasema hayo katika mazungumzo ya simu na Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia. Wawili hao wamejadili kuhusu matukio ya karibuni katika eneo pamoja na masuala ya kimataifa yanayohusiana na vita vilivyolazimishwa na Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran.
Katika mazungumzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefafanua kuhusu mashambulizi ambayo yamefanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Iran katika kipindi cha siku 37 zilizopita. Mashambulizi hayo, amesema, yamelenga miundombinu ya viwanda na uzalishaji, hospitali, shule, maeneo ya makazi, pamoja na vituo na taasisi za nyuklia za Iran. Amesisitiza haja ya hatua za haraka kutoka kwa taasisi husika za kimataifa, hasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), ili kulaani vitendo hivyo na kuwawajibisha waliotekeleza mashambulizi hayo.
Aidha Araqchi ameashiria vitisho vya Marekani kuhusu uwezekano wa kushambulia miundombinu ya nishati ya Iran, akisema kauli hizo ni kukiri wazi nia ya kufanya uhalifu wa kivita.
Araqchi ametoa wito kwa pande zote zenye ushawishi ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua msimamo wa kuwajibika unaozingatia sheria za kimataifa, na pia kuzuia matumizi ya Baraza hilo kama chombo cha kisiasa na Marekani.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov amekumbusha msimamo wa kimsingi wa nchi yake wa kulaani uchokozi wa kijeshi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran. Amesisitiza pia umuhimu wa kusitishwa kwa mashambulizi yasiyo halali dhidi ya maeneo ya kiraia, hususan Kituo cha Nyuklia cha Bushehr, na akatoa wito wa kutumia kila fursa iliyopo ili kuzuia kuenea kwa mgogoro huo.