Maria Zakharova, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, ametangaza kuwa Moscow inalaani vikali mashambulio ya hivi karibuni dhidi ya kituo cha Nyuklia cha Bushehr kilichoko kusini mwa Iran.

Kwa mujibu wa taarifa ya IRIB ikinukuu RT, Zakharova amesisitiza upinzani mkali wa Russia dhidi ya shambulio hilo ambalo limefanywa na muungano wa kivita wa Marekani na utawala haramu wa Israel.

Zakharova pia amewasilisha salamu za rambirambi kwa familia ya mmoja wa wafanyakazi wa kiwanda hicho ambaye ameuawa katika tukio hilo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameongeza kuwa vitendo “visivyo halali na visivyo na hekima” ni doa lisilofutika katika hadhi ya kimataifa ya wale waliotokeleza hujuma hiyo.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, baada ya shambulio jipya dhidi ya kiwanda cha Bushehr, ameandika katika mitandao ya kijamii kuwa: Je, mnayakumbuka yale matamshi makali na ya kina yaliyotolewa na nchi za Magharibi kuhusu mapigano karibu na kituo cha nyuklia cha Zaporizhzhia nchini Ukraine? Ameongeza kuwa: Sasa, Marekani na Israel zimelenga kwa bomu Kiwanda cha Bushehr, mara nne.

Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran ameonya kuwa: “Iwapo kutatokea mionzi ya kinyuklia, athari zake hazitamalizikia Tehran pekee, bali zinaweza kukumba pia miji mikuu ya nchi za Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi (GCC).

Aidha, amebainisha kuwa mashambulio dhidi ya miundombinu ya petrokemikali ya Iran yanaonesha wazi malengo halisi ya hatua hizi. Alikuwa akiashiria hujuma dhidi ya viwanda kadhaa vya petrokemikali ambavyo zimefanywa na utawala haramu wa Israel na Marekani katika maeneo ya kusini mwa Iran.

Kwingineko, Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) limetangaza kuwa litatumia njia za kisheria kuchunguza kesi zinazohusiana na uzembe wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), Rafael Grossi, kufuatia mashambulio ya Marekani na Israel dhidi ya maeneo ya nyuklia ya Iran.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye akaunti yake ya X, shirika hilo limesema kuwa kulaani mashambulio dhidi ya maeneo ya nyuklia ya Iran yanayotumika kwa amani, ni jambo la kiwango cha chini kabisa linalotarajiwa kutoka kwa IAEA, ndani ya mfumo wa majukumu yake ya kisheria.

Taarifa hiyo, ambayo imetolewa baada ya shambulio la nne la Marekani na Israel dhidi ya kiwanda cha nguvu za nyuklia cha Bushehr katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, imesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu pia itachunguza ulinzi wa haki zake za kinyuklia na kutathmini sababu za uzembe wa Grossi kuhusu ukiukwaji huo kupitia njia za kisheria.

Majengo mengine yaliyolengwa katika mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel ni pamoja na kituo cha urutubishaji wa urani cha Natanz kilichoko Isfahan, kiwanda cha keki ya njano cha Ardakan katika jimbo la Yazd, pamoja na kituo cha maji mazito cha Khondab kilichoko Arak.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *