Washington/Tehran. Mwanajeshi wa anga wa Marekani aliyekwama nyuma ya mstari wa adui baada ya ndege ya kivita kuangushwa ameokolewa katika operesheni ya kishujaa iliyohusisha hatari kubwa.

Rais wa Marekani, Donald Trump, amesifu operesheni hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita, akieleza kuwa ni “moja ya operesheni za utafutaji na uokoaji zilizo za kuthubutu zaidi katika historia ya Marekani.”

Mwanajeshi huyo alikuwa pamoja na rubani ndani ya ndege ya kivita aina ya F-15 iliyodunguliwa juu ya eneo la mbali nchini Iran Ijumaa iliyopita.

Rubani alifanikiwa kujinusuru kwa kuruka nje ya ndege na kuokolewa siku hiyo hiyo kwa msaada wa helikopta mbili za kijeshi, lakini mwenzake alibaki na kupotea kwa muda.

Kwa mujibu wa Trump, mwanajeshi huyo aliyepotea, ambaye ni kanali mwenye heshima kubwa, alifanikiwa kujificha na kukwepa vikosi vya Iran kwa takriban siku mbili huku akilindwa na ndege zisizo na rubani (drones) aina ya Reaper zilizokuwa zikizunguka angani.

Akiwa na bastola pekee kwa ajili ya kujilinda, kanali huyo alijificha katika mazingira hatarishi kabla ya kufanya juhudi za mwisho za kukimbilia eneo la uokoaji.

Kwa mujibu wa Daily Mail, operesheni hiyo tata ilihusisha mamia ya wanajeshi maalumu pamoja na makumi ya ndege za kivita na helikopta.

Katika hatua ya uokoaji, ndege mbili za uokoaji zilikwama katika uwanja wa ndege wa mbali ndani ya Iran na zililipuliwa makusudi ili zisikamatwe na adui.

Kanali huyo alilazimika kujificha kwa saa 36 ndani ya ardhi ya Iran katika mazingira magumu, huku akiepuka kukamatwa.

Wakati huohuo, taarifa zilisema wananchi wa Iran walikuwa wameahidiwa zawadi ya Dola 60,000 za Marekani (Sh156 milioni) kwa yeyote ambaye angemkamata mwanajeshi huyo wa Marekani.

Ili kumlinda, ndege za kivita za Marekani zilirusha mabomu na silaha kuwazuia wanajeshi wa Iran wasimkaribie.

Vikosi vya Marekani vilipokaribia eneo alilokuwapo, mapigano makali yalizuka kati yao na wanajeshi wa Iran.

Hatimaye, ndege tatu za uokoaji ziliondoka Iran kuelekea Kuwait na kukamilisha operesheni hiyo muda mfupi kabla ya saa sita usiku.

Trump alithibitisha kuwa kanali huyo amejeruhiwa, lakini “atakuwa sawa,” akieleza kuwa ushindi huo umetokana na hali iliyokuwa ngumu.

Amesema hii ni mara ya kwanza katika historia ya kijeshi ambapo marubani wawili wa Marekani wanaokolewa tofauti ndani ya eneo la adui, akisisitiza kuwa hakuna mwanajeshi wa Marekani atakayeachwa nyuma.

Aidha, amesema makumi ya ndege zenye “silaha hatari zaidi duniani” zilitumwa kuhakikisha uokoaji huo unafanikiwa.

“Shujaa huyu alikuwa nyuma ya mistari ya adui katika milima hatari ya Iran, akifuatiliwa na maadui wetu waliokuwa wakimkaribia kila saa,” amesema Trump kupitia mtandao wa Truth Social.

Kwa mujibu wa Fox News, mafanikio ya operesheni hiyo yalichangiwa pia na mkakati wa udanganyifu uliotekelezwa na CIA ndani ya Iran, ambapo ilienezwa taarifa kuwa tayari mwanajeshi huyo amepatikana na kuhamishwa, jambo lililochanganya vikosi vya Iran.

Mwanajeshi huyo aliruka kutoka kwenye ndege ya F-15E pamoja na rubani wake mapema Ijumaa, tukio lililosababisha operesheni kubwa ya kumtafuta iliyodumu kwa siku mbili na kuishia katika mapigano makali.

Trump amesema rubani wa ndege hiyo aliokolewa kwa siri saa chache baada ya ajali ili kutoathiri operesheni ya pili ya uokoaji.

Ameongeza kuwa operesheni zote mbili zilifanyika “bila hata Mmarekani mmoja kuuawa au kujeruhiwa.”

Hata hivyo, vyombo vya habari vya Iran viliripoti kuwa watu watano waliuawa katika mashambulizi yaliyofanywa wakati wa operesheni hiyo.

Ndege ya F-15E iliangushwa Ijumaa iliyopita, muda mfupi baada ya ndege nyingine ya Marekani aina ya A-10 pia kudunguliwa na vikosi vya Iran, ikiwa ni mara ya kwanza kwa ndege za Marekani kuangushwa tangu vita hivyo vianze.

Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) kilijinasibu kwa shambulizi hilo na kusambaza picha za ndege zilizoanguka kupitia vyombo vya habari vya serikali.

Aidha, ubalozi wa Iran nchini Afghanistan ulitoa picha mpya zikionesha mabaki ya ndege hiyo yakiwa yameungua vibaya, ukieleza kuwa teknolojia iliyodaiwa kuwa “haionekani wala kushambuliwa” sasa imeangushwa.

Picha hizo zilionesha mabaki ya ndege hiyo yakiwa yameenea katika eneo kubwa lisilo na watu, zikiwa ni ushahidi wa mapambano makali yanayoendelea kati ya pande hizo mbili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *