.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 5

Ripoti zinasema kuwa rubani wote wawili wa ndege ya Marekani aina ya US F-15 iliyodunguliwa na Iran wameokolewa, hii ikiwa moja wapo ya misheni ya kipekee ya uokoaji kufanywa na jeshi la Marekani katika historia yake ya miongo kadhaa ya vita.

Kwa mujibu shirika la habari la CBS, rubani wa pili pia aliokolewa kupitia mojawapo ya oparesheni ngumu zaidi.

Oparesheni ya uokoaji

Nchini Marekani, vikosi maalum vya anga hupewa mafunzo ya kufanya oparasheni kama hizi za kipekee za uokoaji wa wanajeshi wanaojipata katika hali tata au kama tukio hili ambapo ndege za kijeshi zinaangushwa na adui.

Ikilinganishwa na oparesheni ambazo hufanyika kutoa misaada kwa binadamu au kuwaokoa watu waliokwama katika maeneo tofauti, oparesheni ya kijeshi hufanyika katika maeneo ambayo kuna mzozo na mapigano.

Kama ilivyotokea nchini Iran, baadhi ya oparesheni hizo hutokea katika ardhi ya adui.

Oparesheni ya utafutaji na uokoaji hufanywa na ndege aina ya helikopta, ikiwa imeambatana na ndege zingine za kuiongezea mafuta na kutekeleza mashambulizi wakati wanashika doria angani huku wakiendeleza oparesheni yao.

Kamanda mmoja wa zamani kikosi maalum cha uokoaji aliambia shirika la habari la CBS kuwa Oparesheni hiyo ya uokoaji kama ile iliyotokea Iran huhusisha angalau wanajeshi 24 wakichunguza eneo la tukio kutumia helikopta za black hawk.

Aliongezea kuwa kikosi hicho huwa tayari kuruka nje ya ndege ikiwa itabidi ili kumtafuta mmoja wao aliyetoweka.

Kulingana na CBS, iwapo mwanajeshi aliyepotea atapatikana, atapewa matibabu hitajika, na kuondolewa katika ardhi ya adui na kuhamishwa hadi eneo salama.

Kamanda huyo wa zamani anasema “hicho ndicho hasa wanachofundishwa kufanya kote duniani. Wanaitwa Swiss Army Knife of the Air Force.”

Video iliyochapishwa kutoka Iran siku ya Ijumaa inaonyesha helikopta za kijeshi za Marekani pamoja na angalau ndege moja ya kujaza mafuta angani zikiendeleza operesheni katika jimbo la Khuzestan.

Muda ni jambo la muhimu sana katika operesheni hizi, kwani vikosi vya Iran vina uwezekano pia wa kuwa vinatafuta mtu au watu hao wa Marekani kwa wakati huohuo.

Jonathan Hackett, aliyewahi kuwa mtaalamu wa operesheni maalum wa Kikosi cha Wanamaji cha Marekani, aliiambia BBC kwamba timu za uokoaji mwanzoni zingetafuta dalili zozote za kuonyesha wanajeshi hao wangali hai.

“Wao huanza utafutaji katika eneo ambalo mtu huyo alionekana mara ya mwisho, kisha kupanua eneo la utafutaji kwa mduara huo, wakizingatia kasi ya mtu huyo kusonga katika hali tofauti na katika maeneo haya yenye mazingira magumu sana.”

Jonathan Hackett aliongeza kuwa aina hii ya operesheni huenda ikawa ni “operesheni isiyo ya kawaida ya uokoaji,” na lazima ifanywe kwa msaada wa vikosi vya eneo hilo. Hii ina maana kwamba makundi ya wenyeji wa eneo hilo huenda tayari wamewasiliana mapema na jeshi la Marekani ili kuratibu mipango ya dharura na kusaidia katika uokoaji.

Alisema kuwa kusini-magharibi mwa Iran ni makazi ya watu wa jamii ya Lor, jamii ndogo ambayo “kihistoria imekuwa ikipinga serikali ya sasa” na huenda ikawa tayari kusaidia wageni kupata njia salama ya kupita.