MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kesho itaanza mchakato wa kupokea maoni ya wadau kuhusu uwezekano wa kufanya mapitio ya nauli za usafiri wa umma, baada ya kupanda kwa bei ya mafuta na wadau kulalamika kunachangia kuongezeka kwa gharama za uendeshaji kwa watoa huduma.

Taarifa ya umma iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo jijini Dar es Salaam imesema bei ya mafuta ya petroli na dizeli imeongezeka kwa takribani Sh 950 kwa lita, hali inayotishia kuathiri utoaji wa huduma za usafiri ikiwa haitapatiwa ufumbuzi wa haraka.

Suluo amesema kuwa endapo mwenendo wa kupanda kwa bei ya mafuta utaendelea, ni wazi kuwa gharama za uendeshaji zitaongezeka zaidi na hivyo kuathiri sekta nzima ya usafiri wa umma, jambo linaloweza kusababisha hitaji la kurekebisha nauli ili ziendane na hali halisi ya kiuchumi.

Amefafanua kuwa Latra kwa kuzingatia Kifungu cha 19 cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413, ina wajibu wa kufanya mapitio ya tozo mbalimbali za huduma za usafiri, ikiwemo nauli, kwa kuzingatia maslahi ya watumiaji na watoa huduma kwa wakati mmoja.

Kutokana na hali hiyo, mamlaka hiyo imeitisha mkutano wa wadau unaoanza kesho Aprili 8, mwaka huu katika Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, kuanzia saa 3:30 asubuhi. SOMA: Latra: Nauli ya Sh 1,000/- mwendokasi ni ya mpito

Suluo amesema lengo ni kukusanya maoni yatakayosaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa. “Maoni ya wadau ni muhimu katika kuhakikisha kuwa nauli zitakazopendekezwa zinaakisi gharama halisi za uendeshaji huku zikilinda maslahi ya wananchi,” alisema Suluo.

Aidha, Latra imeeleza kuwa wadau watakaoshindwa kuhudhuria mkutano huo ana kwa ana watapata fursa ya kushiriki kwa njia ya mtandao kupitia Latra Online TV, huku wale watakaotaka kuwasilisha maoni yao wakihimizwa kuyatuma kupitia barua pepe rasmi za mamlaka hiyo.

Kwa mujibu wa Kanuni za Tozo za Latra za mwaka 2020, mchakato wa mapitio ya nauli unaweza kuanzishwa na mtoa huduma au mamlaka yenyewe pale inapobidi, ili kuhakikisha huduma za usafiri zinaendelea kuwa endelevu bila kuwaumiza watumiaji. Kupanda kwa bei ya mafuta kumetokana na athari ya vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *