Dar es Salaam. Mwimbaji Faustina Mfinanga maarufu Nandy amemsaini na kumtambulisha mwanamuziki mpya ndani ya The African Princess ukiwa ni mwendelezo wa kuwainua wasanii wa kike kupitia lebo yake hiyo ambayo tayari imeacha alama.
Pipi Jojo, binti mdogo kabisa mwenye kipaji kikubwa cha muziki ndiye msanii mpya ndani ya The African Princess, lebo ambayo inajihusisha na wasanii wa kike pekee, na hata jina lake linasadifu hilo.
Hatua hii mpya imekuja baada ya mwaka uliopita lebo hiyo kuachana na Yammi kwa kile kilichotajwa kama makubaliano ya pande zote mbili, ikiwa ni baada ya kufanya kazi pamoja kwa takribani miaka miwili.
Nandy, mshindi wa Trace Awards 2025, ameweka nguvu katika kuwainua wasanii wengine baada ya kulijenga vilivyo jina lake na sasa akiwa ni miongoni mwa wasanii wenye nguvu kubwa ya ushawishi hapa Afrika Mashariki.
Ikumbukwe Nandy alitoka kimuziki takribani miaka 10 iliyopita kupitia wimbo wake Nagusagusa (2016) uliotayarishwa na Emma The Boy chini ya Tanzania House of Talent (THT).
Video ya wimbo huo ambayo iliongozwa na Director Hanscana, ilitoka Julai 22, 2016 ikiwa ni takribani miezi minne tangu Nandy kushika nafasi ya pili katika shindano la kwanza la karaoke Afrika, Tecno Own The Stage.
Baada ya kuachia albamu yake ya kwanza, The African Princess (2018) ambayo ilifanya vizuri ndipo na lebo ikazaliwa ikitumia jina hilo hilo ingawa kwa wakati huo ilianza kwa kusimamia kazi zake tu.
Miaka mitano baadaye, ndipo The African Princess Label ikamtambulisha msanii wa kwanza ambaye ni Yammi aliyekuja na Extended Playlist (EP), Three Hearts (2023) yenye nyimbo tatu huku akiwa hajamshirikisha msanii yeyote.
Kwa muda mfupi chini ya The African Princess Label, Yammi akawa mwanamuziki mkali akitamba na nyimbo zake kama Namchukia (2023), Tiririka (2023), Nitadumu Nae (2024), Kukupenda (2024) na kadhalika.
Kubwa zaidi, Yammi alikuwa msanii wa tatu wa kike Bongo aliyesikilizwa (most streamed) zaidi katika mtandao wa Boomplay Music 2023 akiwa ametanguliwa na Zuchu na Nandy.
Alitumbuiza na kuwania tuzo za muziki Tanzania (TMA), kama Msanii Bora Chipukizi kupitia wimbo wake Namchukia (2023) ambao video yake hadi sasa imetazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 5.8.
Hadi anaondoka katika lebo hiyo mnamo Mei 2025, Yammi tayari alikuwa ni mwanamuziki maarufu huku akiwa ameshirikiana na Nandy katika wimbo mmoja, Lonely (2024) uliotayarishwa Mafeeling Records.
Sasa Pipi Jojo ndiye anaenda kuvaa viatu vya Yammi ndani ya The African Princess, bila shaka Nandy ameshajiridhisha na uwezo wake na kuona anaweza kuibeba vilivyo chapa ya lebo hiyo na kuitangaza zaidi.
Hata hivyo, moja ya mtihani ambazo Pipi Jojo anaweza kukutana nazo ni baadhi ya mashabiki kutaka kumshindanishwa au kulinganisha matokeo ya kazi yake na kile ambacho Yammi alishakifanya katika lebo hiyo.
Uzuri ni kwamba Pipi Jojo tayari uwezo wake unajulikana kupitia nyimbo chache alizoachia chini ya menejimenti ambayo awali alikuwa anafanya nayo kazi kabla ya kuachana katika mazingira ambayo hayaeleweki vizuri.
Hivyo tunaweza kusema Pipi Jojo ni sawa na Yammi ambaye kabla ya kusainiwa na Nandy tayari alisharekodi baada ya kushirikishwa na RJ The DJ (Romy Jons) katika wimbo wake Sina (2022).
Ikumbukwe Nandy si msanii wa kwanza wa kike Tanzania kuanzisha lebo na kusaini msanii, alifanya hivyo Vanessa Mdee (Mdee Music), Shilole (Shishi Gang), Shaa (SK Music), Wema Sepetu (Endless Fame Label), Hamisa Mobetto (Mobetto Music) na kadhalika.
Hata hivyo, lebo hizo nyingi zimekuwa hazifanyi vizuri sokoni na hufa mapema kabla ya kufanikisha chochote kikubwa au kufikia lengo la msingi la kuanzishwa kwake.
Mathalani Mdee Music iliwasaini wasanii wawili, Mimi Mars pamoja na Brian Simba, lakini baada ya Vanessa kuacha muziki, lebo nayo ikasimama kufanya kazi na hadi sasa hakuna kinachoendelea.
Mnamo Juni 2020, Vanessa alitangaza kuachana na muziki wa Bongofleva kwa kile alichodai alikuwa akiwekeza fedha, nguvu na jitihada kubwa lakini kile alichokuwa anapata haviendani na matarajio yake, kitu kilichomfanya kuishi kwa msongo wa mawazo.