
Musoma. Washtakiwa watatu katika kesi ya mauaji ya Rhoda Mobe, mkazi wa Kijiji cha Burunga wilayani Serengeti, wamehoji kuchelewa kwa upelelezi wa kesi yao, wakidai umevuka muda wa kisheria wa siku 90 tangu kukamatwa kwao.
Washtakiwa hao ni Simon Ruhinda (55), muhudumu wa ofisi katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Marco Maginga (45), mwalimu wa shule ya msingi jijini Mbeya na Mwita Maginga (47), mkulima mkazi wa Tarime.
Wakizungumza leo Aprili 13, 2026 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, washtakiwa hao wameeleza kutoridhishwa na sababu za upande wa mashtaka kuendelea kudai upelelezi haujakamilika kila wanapofikishwa mahakamani.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Marco Maginga amesema muda mrefu umepita tangu wakamatwe, hivyo wanahitaji maelezo ya msingi kuhusu kuchelewa kwa upelelezi huo.
“Tunataka kujua ni kwa nini upelelezi haujakamilika hadi sasa wakati muda wa kisheria umepita. Kila tukija mahakamani tunaambiwa bado haujakamilika,” amesema.
Hata hivyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Eugenia Rujwahuka amesema ufafanuzi kuhusu suala hilo utawasilishwa kwa washtakiwa kupitia wakili wao, ambaye hakuwepo mahakamani siku hiyo.
Ameuagiza upande wa mashtaka kuwasiliana na wakili wa utetezi ili kutoa maelezo ya kina kuhusu sababu za kuchelewa kwa upelelezi.
“Ni kweli upelelezi umechukua muda mrefu tangu Desemba hadi sasa. Upande wa mashtaka watawasiliana na wakili wenu ili mpate majibu,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 28, 2026, itakapotajwa tena.
Awali, Wakili wa Serikali, Joyce Matimbwi ameomba kesi hiyo ipangiwe tarehe nyingine kwa kuwa upelelezi bado unaendelea.
Washtakiwa wanakabiliwa na shtaka la mauaji kinyume cha Kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu. Inadaiwa walimuua Rhoda Mobe kwa kumkata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya kuvamia nyumbani kwake usiku wa Oktoba 23, 2025.
Kutokana na uzito wa shtaka hilo, washtakiwa wote wanaendelea kushikiliwa mahabusu, huku Mahakama ya Hakimu Mkazi ikikosa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.