
DODOMA: Serikali imeeleza kuwa inaendelea kujenga shule za sekondari katika kata mbalimbali nchini ili kuwapunguzia umbali wanafunzi kote nchini wakiwemo wa Wilaya ya Kisarawe.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Festo Dugange wakati akijibu swali la Mbunge wa Kisarawe, Selemani Jafo aliyehoji ni lini Serikali itatenga fedha za ujenzi wa Shule ya Sekondari eneo la Mafizi ili kupunguza umbali kwa Wanafunzi wa Mafizi na Nyani.
Naibu waziri katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22 – 2023/24 serikali imejenga shule mpya tano za sekondari ikiwemo shule ya Dk. Selemani Jafo, Kitanga Kisarawe, Muungano Boga, Visiga na Vitende katika Halmashauri ya Kisarawe kwa gharama ya shilingi bilioni 1.83.
Ameeleza kuwa wanafunzi wanaotoka Mafizi na Nyani wanasoma katika shule ya Sekondari Gwata Kisarawe kata ya Mafizi hivyo ili kuwaondolea changamoto ya umbali Serikali katika mwaka wa fedha 2025/26 imepeleka shilingi milioni 68 .681 kwa ajili ya ukamilishaji wa bweni ambapo kwa sasa liko hatua ya plasta.