Wavuvi katika Kaunti ya Busia, Magharibi mwa Kenya, sasa wanakumbatia ufugaji wa samaki kwenye Vizimba, na kuachana na mfumo wa zamani ili kukabiliana na uhaba wa samaki kwenye ziwa Victoria.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Mwandishi wetu Petronila Ogalo, amewatembelea wavuvi hao katika eneo la Port Victoria na hii hapa ni ripoti yake..
Katika ufukwe wa Mulukoba nakutana na wavuvi, ambao wamefunga kazi ya siku baada ya saa nyingi kwenye Ziwa Victoria.
Tangu walipoanza kutumia mfumo huu wa vizimba, Conrad Musungu mmoja wa wavuvi anaeleza mabadiliko wanayoyaona.
”Uvuvi wa vizimba umebadilisha maisha yangu, umenihakikisha pato la kila siku na usalama wangu baharini haswaa kutoka kwa mashambulizi ya kila mara kutoka kwa maafisa wa taifa la Uganda” amesema Conrad Musungu – Mvuvi.
Joackim Omollo Mwenyekiti wa wavuvi, katika fukwe hii ya Mulukoba, anaeleza licha ya mafanikio ya ongezeko la samaki, wanakabiliwa na changamoto.
”Mfumko wa bei ya vyakula vya samaki umeathiri sana mapato yetu kama wavuvi na pia hatuna mashine za kupima viwango vya samaki wachanga, mara nyingi tunanunua samaki wachanga elfu tano ila wakati wa mavuno tunapata ni elfu tatu au hata mbili.” Joackim Omollo Mwenyekiti wa wavuvi – Mulukoba.
Upatikanaji wa soko la uhakika wa samaki hawa, ni changamoto nyingine kubwa inayowakumba wavuvi hawa
“Tungependa serikali ya kaunti ya Busia iweze kuwekeza kwa kutafuta soko kwa mavuno yetu ili kurahisisha kazi ya ukulima wa samaki na kuzuia hasara zinazotokana na ukosefu wa samaki.”
Tangu mwaka 2018, tangu matumizi ya vizimba yalipoanza kutumiwa na wavuvi hapa Busia, vimeongezeka na kufikia 365 na kuongeza kiwango cha samaki.
Petronila Ogalo, Busia, RFI Kiswahili