
Mapigano mapya yameshuhudiwa tena Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, siku mbili baada ya mazungumzo mapya kati ya waasi wa M23/AFC na serikali ya Kinshasa, kukamilika nchini Uswizi ambapo pande zote ziliahdi kuheshimu maelewano ya kusitisha vita.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Mapigano hayo yameripotiwa katika vijiji vya Mikenge, Kakenge, Point zéro, Kalingi na Bidegu.
Dria Nyamanyonga ni mkazi wa Minembwe.
“Tuliona vita Minembwe lakini huu mwaka tunaona yale ambayo hatujawahi kuona. Vita vya ndege zisizokuwa na rubani. Hatuondoki ndani ya nyumba.” Alisema Dria Nyamanyonga, mkazi wa Minembwe.
Semahoro Karaha, ni Msimamizi wa watu mashuhuri wa Minembwe, anaonya Umoja wa Mataifa kuliangalia suala hili kwa ukaribu.
“Ndege zisizo na rubani zinashambulia ngombe, nyumba za watu.” Alisema Semahoro Karaha, ni Msimamizi wa watu mashuhuri wa Minembwe.
Kupitia ujumbe mbalimbali uliosambazwa tangu mwanzo wa mwaka huu katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa Kinshasa, baadhi ya viongozi wa jamii ya Banyamulenge wamewataka ndugu zao kutokubali ushawishi wakikabila unaojaribu kuwatenga.
Enock Sebineza ni mmoja wa watu mashuhuri wa Banyamulenge wanaoishi Kinshasa.
“Jamii zote zisikubali shinikizo la Rwanda la kuchochea ghasia ili baadhi ya watu wainuke dhidi ya wengine. Hakika tuna migogoro na matatizo na majirani zetu, lakini Rwanda siku zote imekuwa ikitumia hali hizi kama fursa ya kucheza nafasi ya zimamoto, ikidai kuwalinda Banyamulenge”. Alieleza Enock Sebineza.
Katika taarifa tofauti, Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na waasi wa AFC/M23 wametuhumiana kwa kuanzisha uchokozi katika vijiji vilivyokaribu na Minembwe licha ya Mazungumzo yaliyoanza hivi karibuni nchini Uswizi.
William Basimike – RFI Kiswahili Bukavu.