
Mtwara. Baraza la Famasi nchini limeonya jamii juu ya hatari ya matumizi holela ya dawa, likieleza kuwa tabia hiyo inaweza kusababisha madhara makubwa kiafya ikiwemo uharibifu wa figo, ini pamoja na kusababisha usugu wa dawa mwilini na kufanya matibabu kushindwa kufanya kazi ipasavyo.
Hayo yameelezwa leo Aprili 22, 2026 mkoani Mtwara, katika zoezi la uhamasishaji jamii juu ya matumizi sahihi ya dawa, ambapo wataalamu wamesema matumizi yasiyo sahihi ya dawa bado ni changamoto kwa baadhi ya wananchi, hali inayohitaji elimu endelevu ili kulinda afya za jamii.
Akizungumza katika zoezi hilo, Mfamasia Mwandamizi kutoka Baraza la Famasi, Arafa Bashir, amesme elimu hiyo inalenga kuwajengea wananchi uelewa wa matumizi sahihi ya dawa ili kulinda afya zao.
“Tunasisitiza wananchi wasitumie dawa bila ushauri wa wataalamu wa afya, ni muhimu kufuata dozi, muda na maelekezo sahihi kama ilivyoelekezwa,” alisema.
Mtaalamu huyo ameeleza mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kutumia dawa ni pamoja na kufuata dozi sahihi, kutotumia dawa za mtu mwingine, na kuepuka kugawana dawa.
Aidha, amefafanua kuwa ni muhimu pia kusoma maelekezo ya dawa kabla ya matumizi, kuzitunza katika mazingira salama na pakavu, pamoja na kuripoti madhara yoyote yanayotokea baada ya matumizi kwa wataalamu wa afya haraka iwezekanavyo.
Baadhi ya wananchi walioshiriki zoezi hilo wameeleza kufurahishwa na elimu hiyo wakisema imewasaidia kubadili mtazamo wao kuhusu matumizi ya dawa.
Abillah Mandava, mkazi wa mtaa Mtepwezi, Manispaa ya Mtwara Mikindani amesema elimu hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa jamii.
“Afya zetu ni bora zaidi, na ni muhimu sisi wananchi tukatambua umuhimu wa kufuata ushauri wa wataalamu wa afya katika matumizi ya dawa,” alisema Mandava.
Naye Mohamed Issa, mkazi wa mtaa wa Majengo, amesema elimu hiyo itamsaidia kubadilisha mtindo wa maisha aliyokuwa nao awali.
“Nilikuwa na tabia ya kutumia dawa bila kupata ushauri wa wataalamu wa afya, lakini sasa nimeelewa hatari zake na nitabadilika,” alisema Issa.
Baraza la Famasi limesema litaendelea kufanya kampeni za elimu katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha jamii inapata uelewa wa kutosha kuhusu matumizi sahihi ya dawa na kuimarisha afya za wananchi kwa ujumla.