
Mkuu wa Ujumbe wa Kulinda Amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) amesema kuwa amekutana na kuzungumza na maafisa wa majimbo kuhusu haja ya kufanyika mazungumzo na kufanya juhudi za pamoja ili kurejesha utulivu wa kudumu na kukabiliana na changamoto za kiusalama mashariki ya nchi.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari huko Bunia, makao makuu ya jimbo la Ituri, James Swan ametilia mkazo umuhimu wa kuendelezwa majukumu ya kikosi cha MONUSCO nchini Kongo huku ujumbe huo ukitoa kipaumbele kwa ulinzi wa raia kufuatia vitisho vya makundi yenye silaha katika majimbo yaliyoathiriwa na machafuko ya mashariki mwa Kongo.
Swan amesema kuwa raia wanaendelea kuathiriwa na machafuko na ukosefu wa amani unaosababishwa na makundi ya waasi na hivyo kulazimisha idadi kubwa ya watu kuhama makazi yao na kusababisha mivutano katika jamii.
Ameongeza kuwa: Ushirikiano wa karibu kati ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa na jeshi la Kongo utaendelea kuwadhaminia ulinzi wa moja kwa moja mamia ya maelfu ya watu waliolazimika kuhama makazi yao kutokana na mchafuko.