
Dodoma. Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Switberti Mkama, ameiagiza Wizara pamoja na taasisi zinazohusika na masuala ya teknolojia kuanza kufuatilia mafunzo ya Tehama yanayotolewa kwa wanafunzi ili kubaini kama yanazaa matokeo chanya, hususan katika kuongeza idadi ya wataalamu wanawake katika sekta hiyo.
Dk Mkama ametoa agizo hilo leo Alhamisi, Aprili 23, 2026, katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wasichana katika Tehama iliyofanyika jijini Dodoma.
Amesema ni wakati mwafaka kwa wizara na taasisi zinazotoa mafunzo kuimarisha ufuatiliaji ili kuboresha nafasi ya wasichana katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
Naibu waziri huyo amesema maagizo hayo yanapaswa kutekelezwa katika pande zote za Muungano, Tanzania Bara na Zanzibar, ili kuwezesha tathmini ya namna wanafunzi wanavyotumia ujuzi wanaoupata baada ya kurejea shuleni na vyuoni.
“Ni wakati sasa wa kuanza ufuatiliaji wa wanafunzi hawa, tukilenga kuhakikisha uwepo endelevu na ukuaji wa kile walichofundishwa baada ya kurejea vyuoni na mashuleni,” amesema Dk Mkama.
Ameongeza kuwa ufuatiliaji huo utasaidia kupanua wigo wa ajira katika sekta ya Tehama kwa wasichana, ambao kwa kiasi kikubwa wanakosa fursa hizo kutokana na changamoto za ukosefu wa usawa wa kijinsia na upatikanaji mdogo wa masomo ya fani hiyo.
Aidha, amesema dunia kwa sasa inahitaji wataalamu wa kike wa Tehama, lakini wengi wanakosa nafasi hizo kutokana na changamoto hizo za kijamii.
Hivyo, amesema ni muhimu kwa taifa kuimarisha ushiriki wao ili kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa kundi hilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso, ameiomba Serikali kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Tehama katika taasisi za elimu, pamoja na kutafuta masoko kwa kazi za teknolojia zinazozalishwa na wanafunzi kupitia mafunzo wanayopata shuleni na vyuoni.
Kakoso pia ameitaka Serikali kuwa makini katika usimamizi wa maudhui yanayofundishwa kwa vijana kuhusu matumizi ya teknolojia, akieleza kuwa kuna haja ya kuzuia maudhui yanayoweza kuchochea machafuko.
“Machafuko mengi ulimwenguni yamechochewa na teknolojia, hivyo ni vyema kuongeza umakini katika usimamizi wa maudhui yanayofundishwa kwa vijana wa Kitanzania ili kuepusha hatari ya machafuko katika taifa letu,” amesema Kakoso.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Janeth Mayanja amewataka wazazi kuhamasisha watoto wa kike kusoma masomo ya Tehama ili kuwawezesha kunufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta hiyo kwa sasa.