Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Evance Bisesagu (47), mfanyabiashara na mkazi wa Bupumula, Kata ya Nyamhongolo, Wilaya ya Ilemela kwa tuhuma za kuchimba mahandaki sita na kuendesha ujenzi wa nyumba ya makazi bila kufuata taratibu za kisheria.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Alhamisi, Aprili 23, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, mtuhumiwa huyo alikamatwa jana jioni Aprili 22, 2026, kufuatia taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu uwepo wa mahandaki hayo yaliyokuwa yakihatarisha usalama wa wakazi wa eneo hilo.
Kamanda Mutafungwa amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mmiliki huyo wa jengo alikuwa akifanya shughuli za uchimbaji na ujenzi bila kuwa na vibali kutoka mamlaka husika wala kutoa taarifa kwa vyombo vya kisheria.
Mbali na mtuhumiwa huyo, polisi pia wanawashikilia watu wawili, Ngasa Kasuka na Hamad Kashinje, waliokuwa wakifanya kazi kama vibarua katika eneo hilo.
Aidha, Jeshi la Polisi linaendelea kuwatafuta mafundi na watu wengine waliodaiwa kushiriki katika uchimbaji na ujenzi wa mahandaki hayo.
Akizungumza na Mwananchi eneo la tukio, Diwani wa Kata ya Nyamhongolo, Safia Mkama amesema alipokea taarifa kutoka kwa mwananchi anayeishi jirani na eneo hilo kuhusu uwepo wa mahandaki hayo.
“Nilimwelekeza kwenda kwa mtendaji wa kata na walipofika eneo la tukio ndipo Jeshi la Polisi lilipigiwa simu na kufika kwa ajili ya hatua zaidi,” amesema Mkama.
Naye mkazi wa Bupumula, Siwema Zefania amesema ujenzi huo ulikuwa unahatarisha usalama wa majirani, hususan watoto.
“Kwa kweli hali ilikuwa hatarishi; mahandaki hayo yako wazi na watoto wangeweza kuanguka kirahisi,” amesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, (DCP) Wilbrod Mutafungwa, akitoa maelezo kuhusu tukio la uchimbaji wa handaki na ujenzi wa nyumba bila kibali katika mtaa wa Bupumula, Kata ya Nyamhongolo, Wilaya ya Ilemela Mkoa wa Mwanza.
Kamanda Mutafungwa ametoa wito kwa viongozi wa serikali katika ngazi mbalimbali kufuatilia kwa karibu mienendo ya watu katika maeneo yao ili kuhakikisha usalama wa jamii unalindwa.
Aidha, amesisitiza kuwa kwa ujenzi wowote unaofanyika, ni lazima vibali vitolewe na mamlaka husika, na yeyote atakayebainika kukiuka taratibu hizo hatua kali za kisheria zitachukuliwa, ikiwemo kusitisha ujenzi husika.