KAIMU Kocha Mkuu wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi’ amesema afya ya kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Aisha Mnunka iko vizuri na hakuna shida kubwa aliyoipata.

Jana Jumatano, Mnunka alishindwa kuendelea na mechi ya Ligi Kuu Wanawake kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar, dhidi ya Fountain Gate baada ya kujigonga kichwa kwenye mlingoti ya goli la wapinzani mara baada ya kufunga bao la pili dakika ya 90.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mgosi amesema baada ya kupata changamoto hiyo, Mnunka aliwahishwa hospitali kupatiwa matibabu na sasa anaendelea vizuri.

Aliongeza, hajapata shida yoyote kubwa ya kiafya, hivyo amepewa mapumziko mafupi kabla ya kurejea tena uwanjani.

“Alipata huduma ya kwanza pale pale, kisha akapelekwa hospitali, tunashukuru yuko salama, hajapata shida yoyote zaidi ya kugonga kichwa tu, tunaamini kama ataendelea vizuri mechi ijayo atakuwepo,” amesema Mgosi.

Juzi Simba Queens ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate Princess dakika za jioni, timu hiyo ilionyesha ushindani mkubwa dhidi ya vinara hao wa ligi.

Akizungumzia hilo, Mgosi aliwapongeza Fountain kwa kuonyesha kiwango hicho akisifu ubora wa kipa wao, Nusra Khamis ambaye aliokoa michomo mitatu ya hatari.

“Fountain walikuja na mbinu nzuri ya kujilinda, nawapongeza sana lakini wachezaji wetu walionyesha ukomavu mkubwa na kuja kuamua mechi dakika za mwisho kwa mipira ya kona,” amesema na kuongeza;

“Pia kipa wao alicheza vizuri sana, nampongeza kwa kuwa kama isingekuwa yeye, Simba tulikuwa tumefunga mabao mapema.”

Simba Queens inaendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo na pointi 40 baada ya kucheza mechi 14, ikishinda 13 na kutoa sare mechi moja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *