
Dodoma. Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo anatarajia kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa wadau wa ushirika unaotarajia kufanyika Aprili 24, 2026 jijini hapa, ukiwa na lengo la kujadili hali ya sekta na mikakati ya kukabiliana na changamoto ya uadilifu katika uendeshaji wa vyama vya ushirika.
Taarifa hiyo imetolewa jana Jumanne Aprili 22, 2026 na Mrajisi na mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dk Benson Ndiege alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mkutano huo.
Dk Ndiege amesema mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano wa wadau wa ushirika katika kulinda masilahi ya wanaushirika, kuimarisha imani ya wadau wa ushirika kwa vyama vya ushirika na kuhakikisha kuwa ushirika unakuwa na chombo imara cha maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
“Katika mkutano huo, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, itazindua kampeni maalumu ya kuimarisha uadilifu na uwajibikaji katika vyama vya ushirika yenye kaulimbiu ‘Linda Ushirika, Chagua Uadilifu,” amesema Dk Ndiege.
Amesema kwenye mkutano huo, wataweka mikakati ya kujenga msingi imara wa uwajibikaji, haki na utawala bora katika sekta ya ushirika.
Amesema Mkutano utahusisha wadau wote wa Sekta ya Ushirika wakiwemo wanachama, viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika, wadau wa haki, taasisi zilizojihusisha na ukaguzi, viongozi wa Serikali, wanasiasa,watoa huduma katika vyama vya ushirika, vyombo vya habari na asasi za kiraia.