
Dodoma. Jumla ya Sh775 bilioni zimeombwa na Wizara ya Katiba katika mwaka wa fedha 2026/27, huku vipaumbele 14 vitakavyotekelezwa kwa wakati huo, ikiwemo kufungua kesi tano za uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
Tofauti na matarajio ya wengi, suala la Katiba mpya limetajwa katika mstari mmoja katika sehemu ya vipaumbele kwamba wanakwenda kutoa elimu ya Katiba kwa wananchi ili watambue Katiba.
Kwa mwaka 2025/26, Wizara hiyo ilipitishiwa Sh687.7 bilioni ambazo zilipewa vipaumbele 10, ikiwemo msaada wa kisheria ambao umegusa idadi kubwa ya wahitaji.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Juma Homera ametoa taarifa hiyo wakati akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/27, ambapo kipaumbele cha kwanza ni utekelezaji wa Dira 2050 inayosisitiza utawala bora, haki na mifumo imara ya kisheria kama msingi wa uchumi imara.
Nje ya ukumbi wa Bunge, Dk Homera ametaja sababu za kwa nini Katiba mpya haikuwekwa kwenye bajeti hiyo, akisema inatokana na umuhimu wake kuwa ilishawekwa kwenye Ilani ya uchaguzi ya CCM, hivyo kwa sasa wanajikita kwenye utoaji elimu.
“Hatuwezi kuliweka hapo moja kwa moja, lakini Watanzania watambue ni jambo muhimu kwetu; ndiyo maana tunakwenda kuwapa elimu wananchi wetu ili watambue umuhimu wa Katiba. Lakini jambo hilo litatekelezwa kwani lipo kwenye Ilani,” amesema Dk Homera.
Baadhi ya vipaumbele vingine ni kuimarisha upatikanaji wa haki na mifumo ya sheria, Mpango wa Taifa wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV), mageuzi ya Sekta ya Sheria (Legal Sector Transformation Programme – LSTP), na malengo ya kujenga sekta ya sheria inayotoa haki kwa wakati, yenye ufanisi wa kutumia teknolojia, na inayochochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Waziri Dk Homera amesema katika mwaka wa fedha 2026/27, Wizara, pamoja na mambo mengine, itasaidia kuimarisha ukuu na maendeleo ya Katiba kwa kuwezesha Katiba kufahamika, kutekelezwa na kuchangia kuleta maendeleo endelevu na utawala bora.
Ametaja kuwa ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa haki kwa wananchi, kuimarisha mifumo ya kisheria na kitaasisi nchini ni kufikisha huduma hadi ngazi ya kata na vijiji, na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma za msaada wa kisheria.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo lingine ni kuanzisha mfumo wa ulinzi wa mashahidi na watoa taarifa za uhalifu kwa kuanzisha divisheni maalum ya ulinzi na kujenga miundombinu salama ya ulinzi. Pia, kuimarisha mfumo wa utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala (ADR) kwa kuongeza matumizi ya usuluhishi, upatanishi, majadiliano na maridhiano, na kupunguza mrundikano wa mashauri mahakamani,” amesema Dk Homera.
Waziri amesema Wizara itaimarisha ushirikiano na taasisi zisizo za kiserikali katika utoaji huduma za kisheria, kusimamia maadili na utawala bora, huku ikilenga kuimarisha nidhamu na uwajibikaji wa taasisi za umma kwa kuweka mifumo madhubuti ya uwajibikaji, kupunguza rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii inatarajiwa kuongeza imani ya wananchi kuhusu mfumo wa haki, kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji, kupungua kwa migogoro na gharama za kisheria, ambako kutaongeza utawala bora na uwajibikaji,” amesema.
Waziri amesema bajeti hiyo itaendelea kukamilisha uanzishwaji wa masjala ndogo mpya za Mahakama Kuu katika mikoa ya Simiyu, Njombe, Lindi, Katavi, Singida na Songwe. Pia kutakuwa na ukaguzi wa magereza 78, vituo vya polisi 37 na mahabusu ya watoto moja.
Maeneo mengine yatakayozingatiwa ni pamoja na maeneo wanamozuiliwa watu katika mikoa 20, na kutathmini hali ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto katika mikoa mitano ya Tanzania Bara.
Katika maoni yao, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria wamesema taasisi nyingi chini ya Wizara hiyo zinakumbwa na changamoto ya majengo ya ofisi, hususan ofisi za mikoa.
Akisoma maoni ya Kamati hiyo, Mbunge wa Newala Vijiji, Dk Yahaya Nawanda, amesema asilimia kubwa ya bajeti ya fedha za maendeleo inayohusu ujenzi wa ofisi hizo haikutolewa kikamilifu, na akapendekeza ili kutatua changamoto hiyo na kufikisha huduma kwa wananchi, Serikali ihakikishe inatoa fedha za maendeleo kikamilifu.
Kamati imesema kuwa mradi wa msaada wa huduma za kisheria unaojulikana kama Mama Samia Legal Aid Campaign ulikuwa na manufaa kwa wananchi, hasa wa hali ya chini, kwa kuwapatia haki zao na hivyo kupunguza malalamiko.
“Ili mradi huo uendelee kuleta tabasamu na matumaini kwa watu, Serikali iuendeleze kwa kuwafikia wananchi mbalimbali, hususan wa vijijini na maeneo mengine ya kimkakati yanayolalamikiwa kukithiri kwa migogoro,” amesema Dk Nawanda.
Katika hatua nyingine, Kamati imelalamikia Kampuni ya Suma JKT kuwa imechelewesha ujenzi wa kituo jumuishi cha kisheria katika mkoa wa Mwanza, kilichoanza ujenzi mwaka 2022 na kutakiwa kukamilika mwaka 2023. Hata hivyo, hadi Machi 2026, ujenzi wake ulifikia asilimia 74 huku wakiwa wamelipwa fedha kwa kiasi cha asilimia 88.
Kwa upande wao, Kamati ya Bunge ya Bajeti imesisitiza ujenzi wa mahakama za mwanzo, ikieleza kuwa takribani asilimia 70.84 ya mashauri yote ya mahakama yanatoka katika ngazi ya mahakama za mwanzo, hivyo ni muhimu kuzijenga na kuziboresha.
Mbunge wa Sumve, Moses Bujaga amesoma maoni ya Kamati hiyo akieleza kuwa kuna upungufu mkubwa wa mahakama hizi, ambapo kuna mahakama za mwanzo 960 ikilinganishwa na idadi ya kata 3,956 zilizopo nchini.
“Hivyo, kuna uhaba wa mahakama za mwanzo takribani 2,996. Mahakama mpya za mwanzo zilizopo hivi sasa kwa kiasi kikubwa zilijengwa kwa fedha za mkopo wa Benki ya Dunia, ambapo mpango wake umekoma,” amesema Bujaga.
Amesema kuna mashauri mengi ya migogoro ya ardhi, akitolea mfano mashamba ya chai yaliyopo Mbeya na Tanga, ambayo kutokana na kuchelewa kutatuliwa kwake yameleta athari hasi kwa wakulima wa zao hilo na kwa zao hilo kwa ujumla.
Kamati hiyo imeishauri Serikali kuruhusu mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya kuwa chini ya mahakama ili kurahisisha upatikanaji wa haki, kwani mara nyingi husababisha mzunguko mrefu wa utoaji haki kwa wananchi hoja ambayo iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Sheria, Dk Damas Ndumbaro.