Dar es Salaam. Swali la mwanaume anatakiwa kufanya tendo la ndoa mara ngapi kwa wiki limekuwa likijadiliwa kwa muda mrefu, huku wengi wakilitafsiri kama kipimo cha “nguvu za kiume”.

Hata hivyo, daktari bingwa bobezi wa magonjwa ya mfumo wa mkojo kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Remigius Rugakingira, amesema hakuna idadi maalumu inayomfanya mwanaume aitwe ana nguvu au hana.

Akizungumza na Mwananchi, Aprili 22, 2026 Dk Rugakingira amesema kiafya mwanaume anaweza kufanya tendo hilo mara tatu hadi tano kwa wiki bila madhara, lakini idadi hiyo inategemea hali ya mwili, aina ya kazi anazofanya na makubaliano na mwenza wake.

“Kuna wanaofanya kazi ngumu, hawa hata mara moja kwa wiki si tatizo. Muhimu ni kuridhishana na kuzingatia afya,” amesema.

Amesisitiza kuwa uanaume haupimwi kwa idadi ya kufanya mapenzi, bali ni mchanganyiko wa mambo mengi ikiwemo afya ya akili, lishe bora, mazoezi na hali ya homoni mwilini.

“Kuna dhana potofu kwamba mwanaume mwenye nguvu lazima awe anafanya mara nyingi, lakini hilo si sahihi. Hata mtu anayejizuia anaweza kuwa na uwezo mkubwa,” amefafanua.

Dk Rugakingira amesema uwezo wa mwanaume unahusisha mfumo mzima wa mwili kuanzia ubongo, mishipa ya damu na homoni ambavyo vinahitaji kuwa katika hali nzuri.

Anabainisha kuwa mawazo, msongo wa akili na uchovu vinaweza kuathiri uwezo wa kusimamisha uume na kufanya tendo kwa ufanisi.

“Kusimamisha uume si suala la kiungo pekee, ni kazi ya ubongo na mzunguko wa damu. Ndiyo maana afya ya akili na utulivu ni muhimu sana,” amesema.

Kwa upande wa lishe, amesema chakula bora chenye virutubisho kamili huchangia kuimarisha afya ya uzazi, huku mazoezi yakisaidia kuongeza mzunguko mzuri wa damu mwilini.

 Pia, ametahadharisha kuwa mitazamo inayotokana na mitandao au picha zisizo halisi imekuwa ikiwapotosha wanaume wengi.

Akizungumzia viashiria vya matatizo ya nguvu za kiume, amesema mwanaume anayemaliza tendo ndani ya chini ya dakika moja anaweza kuwa na tatizo la kumwaga mbegu mapema (premature ejaculation), huku kushindwa kabisa kusimamisha uume nako ni changamoto inayohitaji ushauri wa kitaalamu.

Aidha, amesema hata tendo linalodumu kwa muda mrefu kupita kiasi, kama zaidi ya saa moja, si hali ya kawaida kiafya.

“Watu wanafikiri kukaa muda mrefu sana ndiyo uanaume, lakini hata hiyo inaweza kuwa dalili ya tatizo,” ameeleza.

Dk Rugakingira pia amegusia suala la umri, akisema mwanaume huwa katika kilele cha uzazi kati ya miaka 16 hadi 40, ambapo mwili wake huwa na uwezo mkubwa zaidi.

Hata hivyo, amesema kadri umri unavyoongezeka, uwezo unaweza kupungua taratibu jambo ambalo ni la kawaida.

Pamoja na hayo, amebainisha kuwa elimu kuhusu afya ya uzazi kwa wanaume bado ni ndogo, tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo mifumo ya jadi kama unyago na jando ilitoa mwongozo wa maisha ya utu uzima.

 “Leo vijana wengi wanatafuta taarifa mtandaoni na mara nyingi wanapata zisizo sahihi, hali inayosababisha mkanganyiko mkubwa,” amesema.

Amehitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa wanaume kutafuta elimu sahihi ya afya ya uzazi kutoka kwa wataalamu, kuzingatia lishe bora, kufanya mazoezi na kujenga mawasiliano mazuri na wenza wao badala ya kujiwekea presha ya kufikia viwango visivyo halisi.

“Kinachomfanya mwanaume kuwa kamili si idadi ya tendo, bali afya yake kwa ujumla na namna anavyoishi,” amesisitiza.

Asili ya nguvu za kiume

Tatizo la upungufu wa nguvu za kiume halitokei kwa siku moja, bali hutokana na mtiririko wa mtindo wa maisha ambao mwanaume huwa nao angali kijana mdogo, wataalamu wameeleza.

Wamefafanua kuwa ili nguvu za kiume zipatikane, mwanaume anatakiwa kutokuwa na hitilafu yoyote katika mfumo wake wa damu, sambamba na magonjwa yanayoathiri mishipa ya damu, lakini pia inahusisha afya ya akili.

Daktari bingwa wa fiziolojia ya homoni na mazoezi kutoka Chuo Kikuu cha Afya, kishiriki cha sayansi Muhimbili (MUHAS), Fredrick Mashili ametaja saikolojia na kwamba ubongo unahusika katika tendo hilo lakini kikubwa ni vichocheo ‘homoni ya kiume’.

Amesema kiwango cha homoni hii huongezeka zaidi nyakati za asubuhi.

“Kwenye uume kuna mishipa mikubwa ya damu, halafu wenyewe upo kama sponji hivyo mwanaume anavyojengeka kisaikojia kuwa tayari kwa lile tendo damu hutoka katika maeneo mengine ya mwili na kushuka chini damu ikienda katika uume hushibisha ile mishipa inatanuka, uume hurefuka na kunenepa na ndipo nguvu za kiume hutokea,” amesema.

Dk Mashili ametaja sababu kubwa inayoleta shida kwa wengi kuwa ni mishipa ya damu, “hapa ndiyo unakutana na dawa za kuongeza nguvu ambazo kazi yake hushusha damu kwenye uume, mwili hauwezi kufanya kazi wenyewe mpaka nguvu ya dawa na ndiyo maana huwa zinaua sana.”

Amesema kabla mtu hajatumia dawa hizo anashauriwa na daktari na kwamba hushauriwa watu wa miaka 60 kwenda juu sababu zina madhara na ukishaanza kutumia kuna uwezekano hutaweza kuwa na nguvu mpaka uzitumie.

Amesema wataalamu waliweka umri huo kwa kuwa kawaida mwanaume akifikia umri huo kiwango cha homoni hiyo hupungua mwilini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *