Dar es Salaam. Kampuni ya Sanlam Allianz Life Insurance (Tanzania) Limited imezindua mpoango wa mafao unaojulikana kama Salama Plan, ili kutoa suluhisho la uhakika wa kipato kwa wastaafu na kupunguza mzigo wa kifedha unaowakabili katika maisha.

Uzinduzi wa mpango huo uliofanyika jijini Dar es Salaam unakuja wakati ambao idadi ya Watanzania wanaoingia kwenye umri wa kustaafu inaongezeka, huku wengi wao wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa kipato endelevu baada ya kuacha ajira au kupunguza shughuli za kiuchumi.

Kupitia Salama Plan, waliojiunga wanapata fursa ya kuweka fedha mara moja na kuanza kupokea malipo ya mara kwa mara kulingana na ratiba wanayoichagua, jambo linalowawezesha kupanga maisha yao ya baadaye kwa uhakika zaidi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa Sanlam Allianz Tanzania, Julius Magabe amesema mpango huo umeundwa mahsusi kukabiliana na hali halisi ya maisha ya wastaafu wengi nchini.

Afisa Mtendaji Mkuu wa SanlamAllianz  Life Insurance Julius Magabe (kulia) akiwa na Kamishina wa Bima Tanzania, Dk Baghayo Saqware (kushoto) wakiwa wameshikilia ufunguo wakati wa uzinduzi bidhaa mpya inayowalenga waastafu. Picha na Mpigapicha Wetu

“Uzeeni unapaswa kuwa muda wa kupumzika, si wa kuwa na wasiwasi. Kupitia Salama Plan, tunawawezesha watu kufurahia matunda ya kazi zao kwa kujiamini, bila hofu ya kutokuwa na uhakika wa fedha,” amesema Magabe.

Alisema mpango huo ni hatua muhimu katika kupanua wigo wa huduma za kifedha jumuishi nchini, akisema faida zake zinakuwa si tu kwa mstaafu mmoja mmoja, bali pia kwa familia na jamii kwa ujumla.

Magabe anasema mpango huo unahakikisha malipo yanaendelea hata baada ya kifo cha mteja ndani ya kipindi cha dhamana kilichochaguliwa, unaleta ulinzi wa kifedha kwa wanufaika, hatua inayoweza kupunguza utegemezi wa kifamilia na migogoro ya kifedha inayotokana na kukosekana kwa kipato.

Kiwango cha chini cha kujiunga cha Sh5 milioni bila ukomo wa kiwango cha juu, hivyo kuufanya mpango huo kufikiwa na makundi mbalimbali, wakiwemo wajasiriamali, wafanyakazi wa sekta binafsi na hata wale wasiokuwa na mifumo rasmi ya pensheni, lakini walioweza kuweka akiba kwa muda.

Magabe alisisitiza kuwa kampuni hiyo imezingatia pia changamoto za kiuchumi zinazoikumba jamii kwa sasa, ikiwemo kupanda kwa gharama za maisha na majukumu ya kifamilia yanayoendelea hata baada ya kustaafu.

“Tunaelewa changamoto zinazowakabili wastaafu wengi, ikiwemo jukumu la kusaidia familia pana. Huu ni wakati wao wa kufurahia maisha bila changamoto ya kifedha,” alisema Magabe na kuongeza kuwa mpango huo unaweka msisitizo kwenye uhakika wa kipato cha muda mrefu na ulinzi wa familia baada ya kustaafu.

Kupitia majadiliano ya kitaalamu yaliyofanyika sambamba na hafla hiyo, wadau walikubaliana kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuhamasisha utamaduni wa kujiandaa mapema kwa maisha ya baada ya ajira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *