Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Malaria Duniani, takwimu mpya zinaonesha mwanga katika vita dhidi ya ugonjwa huo, baada ya vifo na maambukizi kupungua kwa kiwango kikubwa ndani ya miaka mitano iliyopita.

Kwa mujibu wa tamko la Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe lililotolewa leo Aprili 25, 2026 idadi ya vifo vinavyotokana na malaria imepungua kwa asilimia 50 kutoka vifo 2,460 mwaka 2020 hadi kufikia vifo 1,231 mwaka 2025.

Wakati huohuo, maambukizi katika jamii yameshuka kwa takribani asilimia 30, kutoka asilimia 8.1 mwaka 2022 hadi asilimia 5.7 mwaka 2025.

Mbali na hilo, wagonjwa wanaothibitika kuwa na malaria katika vituo vya afya wamepungua kwa zaidi ya nusu, kutoka watu milioni 6 mwaka 2020 hadi milioni 2.8 mwaka 2025.

Idadi ya wagonjwa wanaolazwa hospitalini kutokana na malaria nayo imepungua kwa asilimia 35 katika kipindi hicho.

Akizungumza katika maadhimisho ya kitaifa yaliyofanyika jijini Dodoma leo Aprili 25, 2026, Dk Magembe amesema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kutekeleza afua mbalimbali za kudhibiti malaria.

Amesema Serikali imeendelea kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba muhimu bila malipo katika vituo vya afya vya umma, hatua iliyochangia kuongeza ufanisi wa matibabu na kupunguza madhara ya ugonjwa huo kwa wananchi.

“Katika miaka ya hivi karibuni, tumeongeza nguvu katika kuzuia maambukizi kwa kudhibiti mazalia ya mbu pamoja na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma kwa wakati. Hii imechangia kupunguza vifo na maambukizi kwa kiwango kikubwa,” amesema.

Aidha, ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2024/25 na 2025/26, Serikali ilitenga jumla ya Sh20 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa afua ya unyunyiziaji wa viuadudu vya kibaiolojia katika mazalia ya mbu. Kupitia fedha hizo, lita 1,250,000 za viuadudu zilinunuliwa na kusambazwa katika halmashauri zote 184 nchini.

Hatua hiyo inalenga kuharibu mazalia ya mbu kabla hawajakomaa na kuanza kusambaza malaria, ikiwa ni moja ya mikakati endelevu ya kudhibiti ugonjwa huo.

Pamoja na mafanikio hayo, Serikali imeandaa Mpango Mkakati wa Taifa wa Malaria wa mwaka 2026 hadi 2030 unaolenga kuimarisha zaidi mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Mpango huo unaweka mkazo katika mikakati sita, ikiwemo kuzuia maambukizi kwa kudhibiti mbu na kuhakikisha wagonjwa wote wanapimwa na kutibiwa kwa wakati.

Dk Magembe amesema ili kufikia lengo la kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030, ushiriki wa jamii ni muhimu, akiwataka wananchi kuchukua hatua za kujikinga na kushiriki kikamilifu katika afua zinazotekelezwa na Serikali.

Miongoni mwa hatua hizo ni kufukia madimbwi ya maji yanayotumika kama mazalia ya mbu, kushiriki katika kampeni za unyunyiziaji wa viuadudu, pamoja na kulala kwenye vyandarua vyenye dawa kila siku.

Amesisitiza pia umuhimu wa wananchi kuwahi katika vituo vya afya wanapopata dalili za malaria ili kupima kabla ya kutumia dawa, akibainisha kuwa siyo kila homa ni malaria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *