
Dar es Salaam. Katika kipindi ambacho Tanzania inaendelea kukabiliwa na changamoto ya ajira kwa vijana, vyuo vikuu vimejikuta katikati ya mjadala mkali kuhusu nafasi yao katika kuwaandaa wahitimu kukabili maisha yao.
Swali ambalo limekuwa likijirudia ni kama taasisi hizi zinaendelea kuwa sehemu ya suluhisho, au zimebaki kuwa sehemu ya tatizo kwa kuzalisha wahitimu wanaotegemea ajira ambazo hazipo.
Miongoni mwa vyuo vinavyoonyesha mwelekeo mpya wa majibu ya changamoto hiyo, ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambacho kimeanza kubadilisha falsafa ya elimu kutoka ya kusoma ili kuajiriwa kwenda kusoma ili kuunda ajira.
Mabadiliko haya hayajitokezi kwa masomo ya darasani pekee bali katika mifumo ya utafiti, ubunifu na uhusiano wa moja kwa moja na mazingira ya nchi.
Mwelekeo mpya UDSM
Katika maadhimisho ya 11 ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu hivi karibuni, takwimu zilizowasilishwa zilionesha kuwa asilimia 19 ya biashara mpya nchini zimeanzishwa na wahitimu wa chuo hicho.
Hii ni ishara kwamba elimu inapounganishwa na ubunifu, inaweza kuzalisha mfumo mbadala wa ajira nje ya sekta rasmi.
Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho anayeshughulikia utafiti, Profesa Nelson Boniface, anaeleza kuwa mabadiliko haya yanatokana na uwekezaji wa makusudi katika utafiti na ubunifu ndani ya chuo.
“Hii imejidhihirisha kwa ukuaji wa ubunifu kupitia machapisho yao, ambapo kwa UDSM tuna ukuaji wa asilimia 11, kiwango cha juu zaidi duniani,” anasema.
Kauli hii inaweka msingi muhimu wa mjadala wa elimu ya juu. Inamaanisha kwamba utafiti hauko tena katika makabrasha ya kitaaluma pekee, bali unazidi kuwa chanzo cha uzalishaji wa mawazo yanayoweza kugeuzwa kuwa biashara na suluhisho za kijamii.
Kwa muda mrefu, vyuo vikuu vilijengwa katika mfumo wa kuzalisha watafuta ajira. Wahitimu wengi walitoka wakiwa na matarajio ya kuingia kwenye ajira rasmi serikalini au sekta binafsi.
Hata hivyo, mabadiliko ya soko la ajira na kasi ya ongezeko la wahitimu, yamefanya mfumo huo kuwa na upungufu mkubwa.
Ndiyo maana mwelekeo unaoonekana UDSM unachukuliwa na wataalamu kama jaribio la kubadilisha falsafa ya elimu yenyewe. Badala ya kuona elimu kama njia ya kupata ajira, inabadilishwa kuwa njia ya kuzalisha fursa.
Simulizi ya Mwami
Kupitia mafunzo ya utafiti na ubunifu, mhitimu wa mwaka 2021, Deus Mwami, ambaye kupitia ubunifu wake wa usanifu na mapambo, ameweza kuingia sokoni kama mjasiriamali.
Kisa chake kinaonyesha jinsi maarifa ya darasani yanavyoweza kubadilishwa kuwa chanzo cha kipato, iwapo kuna mfumo unaowezesha ubunifu kujenga biashara inayolipa.
Mabadiliko ya muundo wa elimu
Katika mtazamo mpana wa elimu, hii inaonyesha kuwa changamoto ya ajira haiwezi kutenganishwa na muundo wa elimu yenyewe.
Ikiwa elimu inaendelea kuwa ya nadharia zaidi kuliko vitendo, basi matokeo yake ni wahitimu wanaoingia sokoni bila ujuzi wa kuunda ajira.
Hata hivyo, mabadiliko haya hayahusiani na wanafunzi pekee, bali sekta ya fedha nayo imeanza kuona mabadiliko haya kama fursa ya kiuchumi.
Kwa mujibu wa Profesa Boniface, taasisi za kifedha kama CRDB Foundation, zimebaini kuwa sehemu kubwa ya wafanyabiashara wadogo wanaofanya vizuri ni wahitimu wa UDSM.
Hali hiyo imechangia kuanzishwa kwa huduma maalumu ya mikopo nafuu kwa wahitimu wa chuo hicho.
Zaidi ya wahitimu 800 tayari wameomba mikopo hiyo, ishara kwamba elimu inapobadilika kuwa ujasiriamali, mfumo wa kifedha nao unalazimika kujipanga upya ili kuendana na mahitaji mapya.
Katika hatua nyingine muhimu, Udsm imeanzisha mfumo wa kuhifadhi kazi za utafiti na ubunifu unaolenga kuhakikisha kwamba matokeo ya tafiti hayabaki katika ngazi ya kitaaluma pekee bali yanatumika na wadau wa maendeleo.
Mfumo huu unaonekana kama daraja kati ya elimu na uchumi. Unabadilisha utafiti kutoka kuwa shughuli ya kitaaluma kwenda kuwa rasilimali ya kiuchumi inayoweza kuingia sokoni na kuleta matokeo ya moja kwa moja.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye, anaeleza kuwa elimu ya juu inapaswa kupimwa kwa uwezo wake wa kuleta mabadiliko katika jamii.
“Tunapaswa kujiuliza tunatumiaje teknolojia katika kuongeza thamani ya elimu na kuboresha maisha ya wananchi,” anasema. Kauli hiyo inafungua mjadala mpana kuhusu mwelekeo wa elimu Tanzania.
Ikiwa elimu haitoi majibu ya moja kwa moja kwa changamoto za ajira, basi inahitaji kubadilishwa ili kuendana na mahitaji ya soko la kisasa.
Kwa hatua hiyo, Udsm inaonekana kama mfano wa taasisi zinazojaribu kuunganisha elimu na uchumi kupitia utafiti, ubunifu, makongamano ya kitaaluma na ushirikiano na sekta binafsi.
Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa mabadiliko haya lazima yaende sambamba na mageuzi ya mfumo mzima wa elimu nchini.
Profesa Boniface anaweka wazi kwamba ubunifu hauwezi kustawi bila mazingira yanayounga mkono utafiti na biashara.
Hivyo basi, changamoto ya ajira kwa vijana haiwezi kutazamwa kama tatizo la soko la kazi pekee, bali kama suala la mfumo wa elimu.
Ikiwa vyuo vikuu vitaendelea kubaki katika mfumo wa zamani, basi tatizo la ajira litaendelea. Lakini ikiwa elimu itabadilika kuwa mfumo wa uzalishaji wa mawazo na biashara, ajira zinaweza kuanza kuzalishwa ndani ya vyuo vyenyewe.