
Licha ya taarifa za kuwepo kwa mazungumzo ya kusaka suluhu ya kidiplomasia, uhusiano kati ya Marekani na Iran unaendelea kuwa tete, huku shinikizo la kiuchumi likiongezwa maradufu.
Marekani imetangaza kuongeza vikwazo vipya, ikisema inachukua hatua madhubuti kuvuruga biashara ya mafuta ya Iran inayodaiwa kufanyika kinyume cha sheria.
Kupitia Wizara ya Mambo ya Nje, Marekani imesema imeweka vikwazo dhidi ya kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta nchini China pamoja na taasisi nyingine 40 zinazodaiwa kuhusika katika mtandao huo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, taasisi hizo zimetajwa kuwa mishipa muhimu ya kifedha kwa utawala wa Iran, zikidaiwa kusaidia kufadhili shughuli zinazotajwa kuleta machafuko katika ukanda wa Mashariki ya Kati.
Hatua hizo zinalenga kukata mtiririko wa fedha unaotokana na biashara ya nishati, ambayo imeendelea kuwa chanzo kikuu cha mapato kwa Iran licha ya kuwepo kwa vikwazo vya kimataifa.
Aidha, Marekani imeahidi kuimarisha zaidi kampeni yake ya shinikizo la kiuchumi dhidi ya Iran pamoja na mtandao wa kimataifa unaodaiwa kuiunga mkono.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Marekani limetangaza kuizuia meli iliyokuwa na bendera ya Iran ikiwa njiani kuelekea bandari ya nchi hiyo, ikiwa ni sehemu ya operesheni za kudhibiti usafiri wa majini.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi hilo, operesheni hiyo ilifanyika Aprili 24, 2026, ikiongozwa na manowari ya kivita ya USS Rafael Peralta.
Jeshi hilo limeeleza kuwa operesheni hiyo inalenga kuzuia usafirishaji unaohusishwa na Iran, hususan biashara ya mafuta ambayo imekuwa mhimili wa mapato ya taifa hilo.
Hatua hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa Marekani wa kukata vyanzo vya mapato vya Iran, huku mvutano kati ya mataifa hayo ukiendelea kuongezeka.
Katika wiki za karibuni, hali imezidi kuwa mbaya zaidi baada ya Marekani kufanya mashambulizi ya kijeshi na Iran kujibu kwa kuchukua hatua katika njia muhimu za usafirishaji wa mafuta.
Moja ya maeneo yaliyoathirika ni Mlango wa Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya kimataifa ya usafirishaji wa nishati, ambapo hatua hizo zimevuruga mnyororo wa usambazaji wa mafuta na kusababisha kupanda kwa bei katika soko la dunia.
Wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanaonya kuwa endapo juhudi za kidiplomasia hazitazaa matunda, mvutano huo unaweza kuendelea kuathiri uchumi wa dunia na usalama wa nishati.