Dar/Arusha. Baada ya kusambaa kwa taarifa kwenye mitandao ya kijamii, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tawi la Olosiva mkoani Arusha kimemfuta uanachama aliyewahi kuwa mgombea uenyekiti wa chama hicho, Odero Odero, ambaye mwenyewe amesema anachukua hatua.

Ikumbukwe Odero aliwahi kugombea nafasi ya uenyekiti wa Chadema Januari 2025 na akashika nafasi ya tatu kwa kupata kura moja. Mwenyekiti wa sasa, Tundu Lissu, alipata kura 513 na Freeman Mbowe alipata kura 482.

Jumla ya kura zilizopigwa katika uchaguzi huo zilikuwa 999, na kura halali zikiwa 996 huku tatu zikiharibika.

Taarifa ya Aprili 23, 2026 ya kufutwa uanachama wa Odero, ambaye alitamba na ajenda yake kuu ya “Mbele kuna mwanga,” imetolewa na Katibu wa Chadema Tawi la Olosiva, nakala ikapelekwa kwa Katibu Kata Olorien na Katibu wa Jimbo la Arumeru Magharibi.

Kulingana na barua hiyo, imerejea Katiba ya Chadema ya mwaka 2006, toleo la 2019, hususan Ibara ya 7.2.11(e) pamoja na Ibara ya 5.4.3.

Aidha, inarejewa kuwa ulipatiwa barua zenye Kumb. Na. CDM/ARM/OLO/ODERO/01 na CDM/ARM/OLO/ODERO/02 ukijulishwa tuhuma zinazokukabili na kuombwa kutoa ushirikiano, hata hivyo umeshindwa kufanya hivyo.

“Kikao halali cha tawi, baada ya kuzingatia masharti ya katiba na Kanuni ya 6.5.1 (a–c), kimebaini kuwa umeenda kinyume na Ibara ya 5.3.3 na Ibara ya 5.3.4 za Katiba ya Chadema,” taarifa imeeleza na kuongeza:

“Kwa mamlaka ya Ibara ya 7.2.11(e) na kwa kuzingatia Ibara ya 5.4.3, tawi linaamua rasmi kukuvua uanachama wa Chadema kuanzia tarehe ya barua hii,” taarifa hiyo imeeleza.

Kulingana na barua hiyo, Odero amepewa haki ya kukata rufaa kwa mujibu wa Ibara ya 5.4.3 ya Katiba ya Chadema.

Kutokana na barua hiyo, Mwananchi ilimtafuta Odero ambaye amesema hata yeye ameiona barua hiyo mtandaoni ikiwa na taarifa zinazofanana na zake.

“Binafsi sina mamlaka ya kuisemea barua hiyo, lakini nitakwenda Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kwa sababu ipo Sheria ya Taarifa Binafsi. Nitaongea na wakili wangu kuchunguza hizo taarifa zinazosambaa.

“Nitaongea na katibu wangu kujua kama anaifahamu hiyo barua. Kama anaifahamu, ndipo tutachukua hatua za kisheria, kwa kuwa zile zinazosambaa ni taarifa zangu binafsi,” amesema.

Ikumbukwe Odero ni mara ya pili anakumbana na kashikashi ndani ya Chadema baada ya Kanda ya Kaskazini, Julai mwaka jana, kumsimamisha katika nafasi ya Katibu wa Kamati ya Sheria na Haki za Binadamu wa chama hicho, kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili.

Taarifa ya kusimamishwa Odero ndani ya Chadema Kanda ya Kaskazini ilitolewa Julai 30, 2025 na Katibu wa Kanda ya Kaskazini, Ndonde Totinan, baada ya kupokea tuhuma dhidi ya kada huyo kuwa na mwenendo usioridhisha.

“Kutokana na uzito wa tuhuma zilizotolewa dhidi yake, na katika kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote mbili, Odero Odero kwa sasa atasimama kuwa Katibu wa Kamati ya Sheria na Haki za Binadamu ili kuipa nafasi ofisi yangu kufanya uchunguzi wa kina juu ya tuhuma dhidi yake,” imeeleza.

“Ikizingatiwa pia, Odero ni mjumbe wa sekretarieti ya kanda yenye mikoa minne ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Hivyo, ili kuondoa mgongano wa kimaslahi, atapisha uchunguzi huru dhidi yake,” imeelezwa kwenye taarifa hiyo.

Totinan amesema suala hilo litawasilishwa katika Kamati ya Maadili ya Kanda, na Odero atapewa fursa ya kujulishwa tuhuma dhidi yake na haki ya kusikilizwa kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama ili kuhakikisha haki inatendeka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *