Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikijiandaa kuungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Serikali imesema watu 3,557 wamepata ajali kazini katika kipindi cha miaka mitatu (2023–2025), huku wengine 169 wakipoteza maisha.
Kwa mujibu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka Aprili 28, na mwaka huu kwa Tanzania yatafanyika mkoani Njombe.
ILO inaeleza kuwa kila mwaka zaidi ya watu milioni 2.93 hufariki dunia kutokana na sababu zinazohusiana na kazi, huku milioni 395 wakipata majeraha makubwa kazini. Aidha, takribani wafanyakazi bilioni 2.41 duniani huathiriwa na joto kali kila mwaka.
Ripoti hiyo pia imebainisha kuwa athari za joto kali na mazingira hatarishi kazini zinaendelea kuongezeka, huku ikikadiriwa kuwa zaidi ya watu 840,000 hufa kila mwaka kutokana na hali za kiafya zinazotokana na hatari za kisaikolojia kazini, zikiwemo kufanya kazi kwa muda mrefu kupita kiasi, ukosefu wa uhakika wa ajira na unyanyasaji mahali pa kazi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu.
ILO inasema hatari hizo zimehusishwa kwa kiasi kikubwa na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu pamoja na changamoto za afya ya akili, ikiwemo msongo wa mawazo na hata kujiua.
Kwa mujibu wa Shirika hilo, athari za kiuchumi za matatizo ya usalama na afya kazini zinakadiriwa kufikia asilimia 1.37 ya pato la dunia (GDP) kila mwaka, kutokana na kupungua kwa uzalishaji, gharama za matibabu na kushuka kwa ufanisi wa wafanyakazi.
Kupitia taarifa ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), ikimnukuu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, Serikali imesema inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa salama na rafiki kwa wafanyakazi.
Waziri Sangu amesema idadi ya vifo na majeruhi kazini inaathiri uzalishaji na uchumi wa taifa, hivyo kuna umuhimu wa kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto hizo.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia OSHA inaendelea kusimamia utekelezaji wa sera na sheria ili kuhakikisha maeneo yote ya kazi nchini yanakuwa na mifumo imara ya ulinzi dhidi ya ajali, magonjwa na vifo.
“Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria ya usalama na afya mahali pa kazi ili kuhakikisha maeneo yote ya kazi yanakuwa salama na yenye mazingira rafiki kwa wafanyakazi,” amesema.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, amewakaribisha wafanyakazi na wadau mbalimbali kushiriki maonesho na huduma zitakazotolewa katika viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema, Njombe.
Naye Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha maadhimisho ya mwaka huu yanafanikiwa ipasavyo kitaifa mkoani Njombe.