Arusha. Aliyekuwa mgombea uenyekiti wa Chadema Taifa, Odero Odero, aliyeshindana na Tundu Lissu na Freeman Mbowe katika uchaguzi uliofanyika Januari 22, 2025, amefukuzwa uanachama huku sababu zikibaki siri.

Katika uchaguzi huo, Lissu aliibuka mshindi kwa kupata kura 513, Mbowe akipata kura 482, huku Odero akipata kura moja.

Taarifa ya kuvuliwa uanachama imetolewa kupitia barua ya Aprili 23, mwaka huu, iliyosainiwa na Katibu wa Tawi la Olosiva, lililopo Kata ya Olorien katika Jimbo la Arumeru Magharibi.

Barua hiyo imerejea vifungu kadhaa vya katiba ya Chadema ya mwaka 2006 (Toleo la 2019) kuwa ndivyo alivyovikiuka.

Imeeleza kuwa Odero alipatiwa barua mbili akijulishwa tuhuma zinazomkabili na kuombwa kutoa ushirikiano, lakini alishindwa kufanya hivyo.

“Kikao halali cha tawi, baada ya kuzingatia masharti ya katiba na kanuni ya 6.5.1 (a–c), kimebaini kuwa umeenda kinyume na ibara ya 5.3.3 na Ibara ya 5.3.4 za Katiba ya Chadema.

“Tawi linaamua rasmi kukuvua uanachama wa Chadema kuanzia tarehe ya barua hii. Una haki ya kukata rufaa kwa mujibu wa ibara ya 5.4.3 ya katiba ya Chadema,” inaeleza barua hiyo, ambayo nakala yake imetumwa kwa Katibu wa Kata ya Olorien na katibu wa jimbo hilo.

Ibara ya 5.4.3 ya katiba ya Chadema inasema endapo uanachama utakoma kwa “Kuachishwa ama kufukuzwa na tawi lake ama ngazi nyingine ya chama, kwa mujibu wa katiba kwa kukosa sifa za kuendelea kuwa mwanachama ama kuwa na mwenendo usioendana na itikadi, falsafa, madhumuni, kanuni, maadili na sera za chama, mwanachama atakuwa  na haki ya kukata rufaa kwa ngazi ya juu kama hakuridhika na adhabu hiyo.”

Hata hivyo, Katibu wa Chadema Jimbo la Arumeru Magharibi, Musa Komondawa, alipoulizwa kuhusu tuhuma zinazomkabili Odero, hakuwa tayari kuziweka wazi. Alisema barua mbili alizopewa ndizo zilizobeba tuhuma hizo, lakini hazikujibiwa.

“Mtu anapofanya makosa au kukiuka katiba, kuna taratibu za kinidhamu ambazo zimewekwa kwa ajili ya kumchukulia hatua,” alisema.

Ameongeza: “Barua mnayoiona ni hitimisho la mchakato uliokuwa umefanyika. Kuna barua ya kwanza na ya pili ambazo zinabeba tuhuma ambazo hazikuwa za hadharani, bali mawasiliano ya ndani kati ya chama na mhusika.

“Bila shaka mnamfuatilia na kumhoji. Msimamo wa taasisi uko wazi; huwezi kuwa mwanachama ukawa na misimamo tofauti na ya taasisi halafu ukaendelea kuwa mwanachama wa chama hicho,” ameeleza.

Kauli ya Odero

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Aprili 25, 2026, Odero amesema hafahamu chochote kuhusu barua hiyo na kwamba ameiona mitandaoni kama ilivyo kwa wengine, hivyo hawezi kuijibu.

“Mimi hiyo barua nimeiona mitandaoni kama ulivyoiona wewe. Kwa kuwa leo siyo siku ya kazi, nitawasiliana na wakili wangu ili kuripoti jambo hilo kwa mamlaka husika.

“Katika taifa hili kuna sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi. Unapoamka na kukuta taarifa zinazofanana na zako, kama majina na namba ya uanachama wa chama cha siasa, ni lazima kuchukua hatua za kisheria,” amesema.

Amesema pia ataandika barua kwa katibu wa Chadema Jimbo la Arumeru Magharibi ili kuthibitisha kama barua hiyo imetoka ofisini kwao.

“Kwa kuwa nimeiona tu mitandaoni na sijui chanzo chake, sipendi kumtuhumu mtu au kujibu jambo ambalo sijathibitisha. Mamlaka husika zitatoa majibu baada ya uchunguzi kubaini nani aliyesambaza taarifa hizo,” amesema.

Awali, taarifa ya kusimamishwa kwa Odero ndani ya Chadema Kanda ya Kaskazini ilitolewa Julai 30, 2025 na aliyekuwa Katibu wa Kanda hiyo, Ndonde Totinan, baada ya kupokea tuhuma dhidi yake za mwenendo usioridhisha.

“Kwa kuzingatia uzito wa tuhuma na ili kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote, Odero atasimamishwa kwa muda katika nafasi yake ya Katibu wa Kamati ya Sheria na Haki za Binadamu, ili kupisha uchunguzi wa kina,” ilieleza taarifa hiyo.

Agosti 13, 2025, Odero alilalamikia kucheleweshwa kwa uamuzi wa tuhuma dhidi yake, huku uongozi ukiahidi kukamilisha mchakato huo ndani ya mwezi huo.

Katika malalamiko yake, alidai kuwa endapo uongozi ungeendelea kukaa kimya, angechukua hatua kupinga anachokiita uonevu, ukandamizaji na udhalilishaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *