Katika taarifa iliyotolewa tarehe 24 Aprili 2026 kutoka Geneva na Mogadishu, shirika hilo limesema ukame sasa unachangia visa vitatu kati ya vinne vya ukimbizi mpya, ikiwa ni ongezeko la asilimia 22 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Onyo la ongezeko la wakaazi kuyahama makaazi yao

Kwa mujibu wa IOM, hata kama msimu wa mvua za Gu (Aprili–Juni) utakuwa wa kawaida au juu ya wastani, watu wengine karibu 125,000 wanatarajiwa kuhama katika robo ya pili ya mwaka 2026.

Mkuu wa Ujumbe wa IOM nchini Somalia, Manuel Pereira, ameonya kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.Amesema ukosefu wa maji, kushindwa kwa mazao na kuporomoka kwa vyanzo vya kipato kunawalazimisha wananchi wengi kukimbia makazi yao kama suluhisho la mwisho, huku jamii zilizo hatarini zaidi zikiathirika kwa kiwango kikubwa.

© FAO/Michael Tewelde Ukame ukitamalaki Oromia na Somalia

Maeneo yaliyoathirika zaidi

Wilaya za Baidoa, Dayniile, Kahda, Diinsoor na Doolow zimeorodheshwa miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi, ambapo ukame umeharibu mazao, kupunguza uzalishaji wa kilimo na kuongeza shinikizo kwa huduma za kijamii ambazo tayari ni dhaifu.

Hali hii imechangiwa na mvua pungufu katika msimu wa Deyr wa mwaka 2025 pamoja na kipindi kikali cha ukame cha Jilaal, hali iliyosababisha vyanzo vya maji kukauka, malisho kuharibika na uzalishaji wa chakula kupungua kwa kiasi kikubwa.

Athari kwa jamii na mifumo ya huduma

IOM imeonya kuwa ongezeko la uhamaji linaweza kuzidisha msongamano katika miji na maeneo yenye huduma, ambayo tayari hayana uwezo wa kuhudumia idadi kubwa ya watu wanaohitaji msaada kwa wakati mmoja.

Familia nyingi zilizokimbia zinalazimika kuishi katika makazi yasiyo rasmi yenye upungufu mkubwa wa maji safi, huduma za usafi wa mazingira na makazi bora.

Aidha, uchunguzi wa hivi karibuni katika eneo la Gedo umebaini kuwa familia nyingi zinasafiri umbali mrefu kutafuta maji, huku vifo vya mifugo vikiongezeka kutokana na ukame na joto Kali,hali inayohatarisha zaidi usalama wa chakula na kipato cha kaya.

UN Photo/Fardosa Hussein Mama na wanawe wakiwa katika hema kwenye makazi ya wakimbizi wa ndani Baidoa Somalia

Hatua za msaada na changamoto zilizopo

Kupitia programu zake za dharura, IOM kwa kushirikiana na wadau wengine wa kibinadamu inaendelea kutoa msaada wa haraka, ikiwemo makazi ya muda, maji, vifaa visivyo vya chakula na huduma nyingine muhimu.Hata hivyo, shirika hilo limesema ukubwa na kasi ya athari za ukame pamoja na uhaba wa chakula vinazidi uwezo wa rasilimali zilizopo, huku makazi ya wakimbizi wa ndani yakikumbwa na msongamano mkubwa na huduma duni.

Wito wa hatua za haraka na endelevu

IOM imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada wa kibinadamu na uwekezaji wa muda mrefu katika miundombinu ya maji, mbinu za kukabiliana na ukame na njia endelevu za kujipatia kipato.

Kwa mujibu wa shirika hilo, hatua hizo ni muhimu ili kusaidia jamii zilizoathirika kukabiliana na majanga ya sasa na kupunguza hatari ya migogoro ya kibinadamu siku zijazo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *