
BEKI wa Fountain Gate Princess, Lucy Pajero amesema kukabiliana na washambuliaji wa Simba Queens, JKT Queens na Yanga Princess ni moja ya changamoto kubwa anayokutana nayo katika ligi hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Pajero amesema timu hizo zina safu kali ya ushambuliaji na wachezaji wenye kasi, nguvu na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, hali inayowapa wakati mgumu mabeki wengi wanaokutana nao.
“Ukweli, mechi dhidi ya Simba na Yanga Princess zinahitaji umakini mkubwa sana. Washambuliaji wao ni wepesi, wana nguvu na wanajua kutumia nafasi chache wanazopata,” amesema Pajero na kuongeza; si rahisi kuwazuia kwa dakika zote 90 bila kufanya makosa, hivyo hulazimika kuwa makini muda wote pamoja na kushirikiana vyema na mabeki wenzake ili kupunguza hatari langoni.
Pajero amesema licha ya ugumu huo, mechi hizo pia humpa nafasi ya kujifunza na kuongeza kiwango chake kutokana na ushindani mkubwa uliopo.
“Ni mechi ambazo zinakujenga kama mchezaji. Unajifunza mengi kwa sababu unakutana na washambuliaji bora zaidi kwenye ligi,” ameongeza.
Kauli ya Pajero inaakisi ushindani mkubwa uliopo kwenye ligi hiyo na timu kubwa zimeendelea kuwa na ushawishi mkubwa kutokana na ubora wa vikosi vyao, hasa safu za ushambuliaji.
Beki huyo alijiunga na Fountain msimu huu akitokea Yanga Princess alipohudumu misimu miwili, ingawa hakuwa akipata nafasi ya kuanza mara kwa mara kikosi cha kwanza.