Kibaha. Katika kuadhimisha miaka 62 ya Muungano, Mkoa wa Pwani leo. April 26, 2026 umepanda miti 620 katika Hospitali ya Wilaya Lulanzi, Manispaa ya Kibaha, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kupanda jumla ya miti 1,120 utakaoendelea kutekelezwa kwa awamu.
Shughuli hiyo imeongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge, akishirikiana na viongozi mbalimbali wa serikali na wadau wa mazingira, ambapo ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira.
Kunenge amesema ni muhimu kwa jamii kutambua kuwa utunzaji wa mazingira ni msingi wa kulinda vyanzo vya maji na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Tunapaswa kulinda mazingira yetu kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na kupanda na kutunza miti, kwa sababu uharibifu wa mazingira una madhara makubwa, ikiwemo kupungua kwa vyanzo vya maji na kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Kunenge.
Ameongeza kuwa baadhi ya wilaya mkoani Pwani tayari zimeanza kuathirika kutokana na uharibifu wa mazingira, hali inayohitaji hatua za haraka na endelevu kunusuru hali hiyo.
Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, amesema mkoa huo umeweka mikakati madhubuti ya kulinda mazingira, ikiwemo kuhamasisha upandaji miti katika taasisi za umma na maeneo ya makazi.
“Mkoa umejipanga kuhakikisha kuwa suala la utunzaji wa mazingira linapewa kipaumbele, ambapo tunahamasisha upandaji wa miti, elimu kwa umma pamoja na usimamizi wa rasilimali za asili ili kuhakikisha uendelevu wa mazingira,” amesema Mnyema.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo wamepongeza juhudi hizo, wakieleza kuwa hatua ya kupanda miti itasaidia kurejesha uoto wa asili na kuboresha hali ya hewa.
Lazaro Musa amesema upandaji miti huo ni ishara ya uwajibikaji wa pamoja katika kulinda mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Ninaamini miti hii itasaidia kurejesha mazingira yetu na kupunguza changamoto za ukame zinazoweza kujitokeza,” amesema.
Kwa upande wake, Lucy Mgimwa amesema juhudi za serikali zinapaswa kuungwa mkono na wananchi wote ili kuhakikisha mafanikio ya muda mrefu.
“Hili si jukumu la serikali pekee, ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha mazingira yanatunzwa kwa faida ya wote,” amesema Mgimwa.