MSHAMBULIAJI wa timu ya taifa ya Twiga Stars na Al Nassr ya Saudia, Clara Luvanga ameingia kwenye kitabu cha rekodi cha wachezaji wa kigeni waliofunga mabao mengi Ligi Kuu Saudi Arabia.
Anayeongoza kwenye listi hiyo ni Iptissam Jraidi raia wa Morocco ambaye katika misimu minne aliyoitumikia Al Ahli amefunga mabao 74, huku 50 yakiwa ya Ligi Kuu Saudia.
Amekuwa mfungaji bora mara mbili mfululizo, msimu wa 2023/24 na 2024/25, anayefuata ni Shokhan Salihi raia wa Iraq aliyefunga mabao 60, mabao 42 amefunga ya kigi kuu na 18 ya mashindano mengine.
Clara anakuwa mchezaji wa tatu wa kigeni kufunga mabao mengi ndani ya ligi hiyo akiweka kambani 62, mabao 56 amefunga ligi kuu na mengine sita ya mashindano mengine Saudia.
Mshambuliaji huyo anaweka rekodi ya kwanza ya kuwa Mtanzania aliyechukua tuzo ya mfungaji bora nje ya nchi na katika misimu mitatu alikuwa kwenye orodha ya wanaowania kiatu cha mfungaji bora.
Mtanzania mwingine aliyewahi kufunga mabao ni Enekia Lunyamila msimu wa 2023/24 akiwa na Eastern Flames na alifunga manane msimu mmoja kisha akatimkia FC Juarez ya Mexico.
Ubora aliouonyesha misimu mitatu tu aliyojiunga na timu hiyo akitokea Dux Lugrono ya Hispania umemfanya kuwa nyota muhimu kwenye kikosi hicho.
Msimu wa kwanza Clara alifunga mabao 11 na asisti saba, uliofuata alifunga 21 na asisti saba na msimu huuu amevunja rekodi ya misimu mitatu akitikisa nyavu mara 24.
Katika mabao 24 aliyofunga aliweka hat-trick tatu, moja alifunga kwenye dabi dhidi ya mahasimu wao, Al Hilal na kuweka rekodi ya aina yake.
Ikumbukwe nyota huyo wa zamani wa Yanga Princess hakuwahi kuchukua kiatu cha ufungaji bora tangu aanze kucheza soka la kulipwa hivyo huu unakuwa msimu wake wa kwanza kubeba kwenye ligi akiwa nje.
Pia hii ni tuzo ya tatu kwa Clara kuchukua akiwa na Al Nassr, kwenye mashindano ya AFC mshambuliaji huyo aliibuka mfungaji bora kwa kuweka kambani mabao matatu sawa na mashindano ya SAFF Women Cup.