
Dar es Salaam. Hali ya uchumi wa dunia inayosababishwa na vita inayoendelea kati ya Marekani na Israel dhidi ya Irani imeanza kuleta athari katika sekta ya afya, hususan upatikanaji wa bidhaa muhimu huku mamlaka zikianza kuweka mikakati ya kukabiliana na hali hiyo.
Mapigano hayo ambayo yameingia zaidi ya mwezi sasa, yamesababisha kuyumba kwa hali ya uchumi duniani ikiwamo bei ya nishati ya mafuta kuadimika na kupanda bei maeneo mbalimbali duniani.
Akizungumza mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Mavere Tukai amesema hali hiyo haiwezi kuepukika, kwani Tanzania ni sehemu ya soko la dunia linalotegemea uzalishaji na usafirishaji wa kimataifa.
“Mtikisiko wa dunia unaoendelea sasa, hata kwenye bidhaa za afya ule mtikisiko hauepukiki. Kuna changamoto za usafirishaji ambapo baadhi ya meli zinaeleza wazi kuwa haziwezi kusafirisha kwa wakati kama ilivyokuwa awali,” amesema.
Ameongeza uzalishaji wa kondomu duniani umeathirika, hali inayoweza kusababisha kupanda kwa bei kati ya asilimia 20 hadi 30, pamoja na ugumu wa upatikanaji wake katika baadhi ya masoko.
“Kwenye uzalishaji wa kondomu tayari wametoa tahadhari kwamba bei inaweza kupanda kwa asilimia 20 hadi 30, na usafirishaji nao unaweza kuwa mgumu zaidi,” amesema.
Hata hivyo, amesema kwa sasa nchi ina akiba ya kutosha ya bidhaa hiyo kwa takribani miezi sita, lakini juhudi zinaendelea kuhakikisha upatikanaji wake unaendelea bila kukwama.
“Sisi tuna idadi ya kutosha kwa miezi sita, lakini sasa inabidi tupambane kuhakikisha tunapata bidhaa hizi kwa wakati ili kuepusha changamoto yoyote inayoweza kujitokeza,” amesema.
Amebainisha ushirikiano na Wizara ya Afya unaendelea kuimarishwa ili kuweka mikakati ya haraka ya kukabiliana na athari za mabadiliko hayo ya kiuchumi duniani.
“Bahati nzuri Wizara ya Afya ipo pamoja nasi katika hili, tunaendelea kushirikiana kuhakikisha huduma za afya haziathiriki kwa kiwango kikubwa,” amesema.
Wataalamu wa afya wanaonya changamoto katika mnyororo wa usambazaji wa bidhaa za afya zinaweza kuathiri upatikanaji wa huduma muhimu, hivyo ni muhimu kuchukua hatua za mapema kuhakikisha upatikanaji endelevu.