Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema Serikali imeanza mchakato wa ujenzi wa ofisi mpya za Mkuu wa Mkoa katika eneo la Magomeni, lililokuwa chini ya umiliki wa DDC, kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi na huduma kwa wananchi.

Chalamila amesema mradi huo utagharimu Sh10 bilioni na utahusisha ujenzi wa jengo la kisasa litakaloendana na hadhi ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na mahitaji ya kiutawala yanayoongezeka.

Kwa sasa ofisi za mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, zipo Ilala Boma, sehemu ambayo ni eneo dogo ambalo halina maegesho ya kutosha, ukumbi wa kisasa wa mikutano na au maeneo ya watu kukaa waskisubiri kupatiwa huduma.

Mkuu huyo wa mkoa ameeleza hayo leo Jumapili Aprili 26, 2026 wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Shule ya Msingi Msimbazi katika ziara ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba jijini Dar es Salaam.

Amesema tayari fedha hizo zimeshaidhinishwa kufuatia maombi ya mkoa huo kuwa na ofisi mpya yenye miundombinu na muonekano unaoendana na hadhi ya jiji hilo linaloongoza kwa shughuli za kiuchumi.

“Tunalenga kuwa na ofisi ya kisasa itakayokusanya huduma mbalimbali za kiutawala chini ya paa moja, ikiwa ni pamoja na ofisi za watendaji, kumbi za mikutano na miundombinu rafiki kwa wananchi,” amesema Chalamila.

Ameeleza uamuzi wa kujenga ofisi hizo eneo la Magomeni unalenga pia kuboresha matumizi ya ardhi na kuinua hadhi ya eneo hilo kihistoria jijini Dar es Salaam.

Chalamila amesema utekelezaji wa mradi huo utaenda sambamba na maboresho ya miundombinu ikiwamo barabara, maji na umeme ili kuhakikisha huduma zinapatikana kwa ufanisi zaidi.

Amesisitiza Serikali imejipanga kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vya ubora vinavyotakiwa, ili kuongeza ufanisi wa utendaji na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *