Dar es Salaam. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema Serikali imekamata madini yenye thamani ya Sh3.31 bilioni, yaliyokuwa yakitoroshwa ndani na nje ya nchi katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026.

Mavunde ameeleza hayo bungeni jijini Dodoma leo, Jumatatu Aprili 27, 2026 wakati wa hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Amesema madini hayo yamekamatwa katika vituo 55 kwenye mikoa ya kimadini ya Kahama, Mwanza, Geita, Dar es Salaam, Arusha, Songwe, Mbeya, Iringa, Mirerani, Mahenge, Chunya, Kagera, Manyara, Mbogwe na Morogoro.

“Madini yaliyokamatwa yalitaifishwa na Serikali na watuhumiwa walifikishwa kwenye vyombo vya sheria. Ni rai yangu kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuzingatia sheria za nchi kuhusiana na biashara ya madini,” amesema.

Mbali na hilo, amesema katika kipindi hicho, jumla ya vibali 8,635 vya usafirishaji madini nje ya nchi vilitolewa, kusafirisha dhahabu, almasi, vito ghafi, vito vilivyokatwa na kusanifiwa, madini ya viwandani, madini ya bati, madini ya shaba na makaa ya mawe.

Vipande vya madini ya dhahabu vyenye thamani ya Sh1.5 bilioni vilivyokamatwa na Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya vikitoroshwa.

Madini hayo yaliyosafirishwa, amesema yana thamani ya Sh9.918 trilioni.

Juhudi hizo, amesema zimechangia kuongeza mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa kutoka asilimia 9.1 mwaka 2023 na kufikia asilimia 10.1 mwaka 2024.

“Hadi kufikia kipindi cha robo tatu ya mwaka 2025, wastani wa mchango wa sekta umefikia asilimia 11.9. Mwenendo huu umechangiwa na kuimarika kwa usimamizi wa sekta na kuongezeka kwa uwekezaji na uzalishaji,” amesema.

Pia, amesema katika kipindi hicho hicho cha Julai 2025 hadi Machi 2026, Tume ya Madini imetoa leseni 454 za madini muhimu na ya mkakati yakiwemo ya kinywe (271), nickel (136), cobalt (2), lithium (6), heavy mineral sands (11) na rare earth elements (28).

Utoaji wa leseni hizo, amesema unaendelea kuweka msingi thabiti wa kukuza uwekezaji katika utafutaji na uendelezaji wa madini muhimu na madini mkakati nchini na kuimarisha jitihada za Serikali za kukuza uchimbaji endelevu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *