Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameishukuru serikali na taifa la Afrika Kusini kwa kuonyesha mshikamano na taifa la Iran.

Rais Masoud Pezeshkian ametoa shukrani zake katika ujumbe uliotumwa kwa Jamhuri ya Afrika Kusini kwa kuonyesha mshikamano na taifa la Iran.

Katika ujumbe huo uliotumwa kwa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, Rais Pezeshkian ameipongeza serikali na taifa la Afrika Kusini kwa maadhimisho ya uhuru wa nchi hiyo, Aprili 27. Ameeleza matumaini kwamba: Katika kivuli cha juhudi za pamoja, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jamhuri ya Afrika Kusini zitapiga hatua katika njia ya kuelekea kwenye ulimwengu usio na ubaguzi, vita, ukoloni, na sera za ubabe.

Afrika Kusini ilitawaliwa na wazungu waliowachache kupitia sera ya ubaguzi wa rangi (apartheid), ambayo ilianza kutekelezwa mwaka 1948. Mfumo huu uliendeleza ubaguzi wa rangi na tofauti za kiuchumi, hali iliyochochea upinzani wa “African National Congress (ANC)” na harakati nyngine za kupinga ubaguzi wa rangi zikiongozwa na watu kama Nelson Mandela na Desmond Tutu.

Kuongezeka upinzani wa ndani, kuzorota uchumi na vikwazo vya kimataifa kuliilazimisha serikali ya ubaguzi wa rangi kuanza mazungumzo ya mageuzi ya kidemokrasia. Apartheid ilimalizika rasmi mwanzoni mwa miaka ya 1990, na Afrika Kusini ilifanya uchaguzi wake wa kwanza wa watu wa rangi zote mwaka 1994, ambapo Nelson Mandela alichaguliwa kuwa rais wa kwanza mweusi wa nchi hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *