Butiama. Serikali wilayani Butiama mkoani Mara, imetangaza kuchukua hatua dhidi ya watendaji wa vijiji, kata na wakuu wa taasisi za umma watakaoshindwa kusimamia utunzaji wa miti inayopandwa katika maeneo yao.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kupunguza hewa ukaa.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Aprili 27, 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Thecla Mkuchika wakati wa kampeni ya upandaji miti ijulikanayo kama, “27 ya Kijani” iliyoratibiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Katika kampeni hiyo, zaidi ya miti 1,000 imepandwa katika Kituo cha Afya Kukirango wilayani humo.

Baadhi ya wakazi wa Kata ya Kukirango wilayani Butiama wakishiriki upandaji wa miti katika kituo cha afya Kukirango. Picha na Beldina Nyakeke

Mkuchika amesema Serikali inaendelea kutekeleza jitihada mbalimbali za kulinda mazingira, ikiwamo kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na upandaji miti na kusisitiza umuhimu wa jamii kuunga mkono juhudi hizo ili kuleta matokeo chanya.

Amesema athari za mabadiliko ya tabianchi zinaonekana wazi, hivyo hakuna budi kuchukua hatua madhubuti, ikiwamo ya kupanda miti kwa wingi na kuhakikisha inakua.

Amesisitiza kuwa viongozi wa taasisi za umma pamoja na watendaji wa vijiji na kata watakaoshindwa kusimamia ipasavyo utunzaji wa miti hiyo, watachukuliwa hatua.

Aidha, Mkuchika amesema Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi ameelekeza kila wilaya kupanda miti milioni 1.5 ili kufikia lengo hilo.

Amesisitiza kuwa upandaji na utunzaji wa miti ni jukumu la lazima kwa viongozi wote wa Serikali na taasisi zake kuanzia ngazi ya vitongoji.

Kwa upande wake, Ofisa Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira wa Wilaya ya Butiama, Emmanuel Makoye amesema tayari wilaya imepanda miti 492,000 kati ya lengo la miti milioni 1.5 kwa mwaka huu na kwamba lengo hilo linatarajiwa kufikiwa kabla ya mwaka kuisha.

Makoye amesema awali wilaya hiyo ilikuwa inakabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa, hali iliyosababisha miti mingi kushindwa kukua kutokana na ukosefu wa mvua.

Hata hivyo, amesema changamoto hiyo imeanza kupatiwa ufumbuzi kupitia utoaji wa elimu ya umwagiliaji.

Baadhi ya wakazi wa Kata ya Kukirango wilayani Butiama wakishiriki upandaji wa miti katika kituo cha afya Kukirango. Picha na Beldina Nyakeke

Amesema wananchi na taasisi mbalimbali wanaelimishwa umuhimu wa kumwagilia miti badala ya kusubiri mvua na kwamba, elimu hiyo imeanza kuleta matokeo chanya.

Baadhi ya wakazi wa Butiama wamesisitiza umuhimu wa kuzingatia zaidi ukuaji wa miti kuliko idadi ya miti inayopandwa.

Mkazi mmoja, Jeremia Muhochi amesema kupanda miti pekee haitoshi bila kuhakikisha inatunzwa hadi ikue na kupendekeza takwimu zitolewe kwa kuzingatia miti iliyokua badala ya iliyopandwa tu.

Naye Nyasige Mbura amependekeza kutungwa kwa sheria ndogo zitakazosimamiwa na Serikali za vijiji ili kulinda mazingira, akisisitiza kuwa suala la mifugo kuharibu miti linapaswa kupewa kipaumbele.

Amesema wafugaji wengi huachia mifugo katika maeneo yenye miti iliyopandwa na kusababisha uharibifu, hivyo kuwepo kwa sheria madhubuti kutasaidia kuwawajibisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *