Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi, amefanya mazungumzo ya simu kwa nyakati tofauti siku ya Jumapili na mawaziri wenzake wa Qatar na Saudi Arabia, ikiwa ni sehemu ya juhudi pana za kidiplomasia za kukomesha mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar ambaye pia ni Waziri Mkuu, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, Araghchi amesisitiza haja ya kuendeleza mashauriano ya kidiplomasia na uratibu wa karibu ili kuunga mkono mipango ya amani na kuimarisha utulivu katika eneo.

Ametoa maelezo kuhusu hali ya sasa, hasa kuhusu usitishaji mapigano ulioratibiwa na Pakistan kati ya Iran na Marekani, pamoja na changamoto za kuudumisha.

Al Thani aliipokea kwa mtazamo chanya hatua ya Iran ya kutumia diplomasia, na akathibitisha kwamba Doha iko tayari kuchukua jukumu la kuongoza katika upatanishi na kurahisisha majadiliano yenye lengo la kukomesha vita dhidi ya Iran.

Katika mazungumzo tofauti, Araghchi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Faisal bin Farhan Al Saud, wamebadilishana maoni kuhusu matukio ya karibuni katika Ukanda wa Asia Magharibi na jitihada zinazoendelea za kidiplomasia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza kwa undani hali ya usitishaji mapigano kati ya Tehran na Washington na kumjulisha mwenzake wa Saudi kuhusu hatua za kidiplomasia za Tehran za kumaliza vita na kupunguza mvutano.

Mapema siku hiyo ya Jumapili, Araghchi pia alizungumza kwa simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan.

Kadhalika, alifanya mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty, ambaye amesisitiza umuhimu wa diplomasia katika kuhakikisha usitishaji mapigano unaendelea kwa njia itakayosaidia kufikia mwisho wa kudumu wa vita.

Mbali na mashauriano na maafisa wa eneo hili, Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Iran pia amezungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot, kuhusu matukio yanayohusiana na usitishaji mapigano.

Araghchi amesisitiza umuhimu wa mataifa ya Ulaya kuchukua nafasi chanya katika mchakato wa kidiplomasia.

Mvutano katika eneo umeongezeka kwa kiasi kikubwa kufuatia vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, vilivyoanza Februari 28 kwa kuuawa kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, na makamanda kadhaa wa ngazi za juu wa kijeshi, raia wa kawaida, wanayasansi na watoto wa shule.

Mnamo Aprili 8, siku arobaini baada ya vita, usitishaji mapigano wa muda uliosimamiwa na Pakistan ulianza kutekelezwa. Mazungumzo yaliendelea Islamabad, lakini hayakufikia makubaliano kutokana na madai yasiyo na mantiki pamoja na masharti ya kupitiliza ya Marekani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *