
Vyama vidogo kumi na viwili vya upinzani nchini Tanzania vimeunda muungano siku ya Jumapili, Aprili 26, ili kufufua mageuzi ya katiba. Mchakato huu ulioanzishwa mwaka wa 2011, umekwama kwa zaidi ya muongo mmoja. Unajumuisha mageuzi yanayolenga kupunguza mamlaka ya rais.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kwa kutoonekana vizuri katika uwanja wa kisiasa, vyama hivi vinataka kutoa sauti zao kwa kutumia suala ambalo limerudi mstari wa mbele katika mjadala kufuatia vurugu za mwaka 2025. Hata hivyo, mpango huu unabaki kuwa mdogo kwani vyama viwili vikubwa, Chadema na ACT-Wazalendo, havihusiki.
Chadema na ACT-Wazalendo zina masharti yao na kwa hivyo kwa sasa si sehemu ya muungano huu. Chadema inadai kuachiliwa huru kwa kiongizi wake, Tundu Lissu, na maafisa wengine, pamoja na mageuzi kwa tume ya uchaguzi. Kwa upande wake, ACT-Wazalendo haitaki kufichua masharti yake lakini pia yanaonekana kukwama.
Vyama kumi na viwili vinavyounda muungano huu vinataka kuharakishwa kupitishwa kwa Katiba mpya nchini Tanzania. Miongoni mwao ni DP, NLD, na UDP, vyama vinavyoshutumiwa mara kwa mara kuwa karibu na serikali. Vyama hivi vinarudia hitimisho la tume kuhusu vurugu za mwaka 2025, ambavyo vinapendekeza kukamilisha mageuzi ndani ya miaka miwili.
Vyama hivi vinaona rasimu hii kuwa muhimu ili kusambaza vyema madaraka miongoni mwa taasisi. Lakini mbali na wito huu, mjadala unazingatia hasa jinsi ya kufanya mageuzi. Je, mchakato uendelee pale ulipoishia mwaka wa 2015, au uanze upya? Na zaidi ya yote, ni nani anayeweka sheria?
Kuna makubaliano kuhusu hitaji la mageuzi ya katiba. Lakini tofauti na mwaka wa 2014, wakati vyama vikuu vya upinzani vilipoungana ndani ya muungano wa UKAWA, muungano huu mpya unaundwa bila vigogo wake wa kisiasa.
“Mabadiliko makubwa katika mazingira ya kisiasa”
Baadhi ya waangalizi wanahoji uaminifu wa mpango huu, wakibaini kwamba vyama hivi viko karibu na serikali. Alipowasiliana na RFI, mtaalamu Thomas Kibwana anasema: “Nadhani si haki kabisa kudharau vyama hivi kumi na viwili kwa sababu tu havijachukua misimamo mikali dhidi ya mamlaka, au kusema kwamba vinaungwa mkono na chama tawala: hakuna ushahidi.”
“Zaidi ya hayo, kama vingeungwa mkono kweli na CCM, bila shaka vingekuwa na ushawishi mkubwa zaidi. Hata hivyo, hivi ni vyama vidogo, vinavyotaka kujipatia jina na kuanzisha uwepo katika uwanja wa kisiasa, katika mazingira ambayo kwa kiasi kikubwa yanatawaliwa na chama tawala,” anaongeza.
Thomas Kibwana anabainisha: “Pia ni muhimu kukumbuka kwamba vyama vingi vinaonekana hasa wakati wa vipindi vya uchaguzi, kisha hutoweka hadi uchaguzi ujao, isipokuwa vyama vichache vikubwa vya kihistoria. Ukweli kwamba baadhi ya vyama hivi—hapo awali havikuwepo baada ya uchaguzi—sasa vinaendelea kushiriki katika mjadala wa umma unawakilisha mabadiliko makubwa katika mazingira ya kisiasa.”