Kibiti. Serikali kupitia ushirikiano na wadau wa afya, ikiwemo Gavi, imekabidhi boti saba zenye thamani ya Sh1.1 bilioni kwa ajili ya kuimarisha huduma za chanjo katika maeneo ya visiwa na mwambao wa Bahari ya Hindi, hatua inayolenga kuwafikia wananchi waliokuwa wakikosa huduma kutokana na changamoto za kijiografia.

Akizungumza leo Jumatano, Aprili 29, 2026, katika Bandari ya Nyamisati wilayani Kibiti Mkoa wa Pwani wakati wa makabidhiano ya boti hizo, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesisitiza matumizi sahihi ya vitendea kazi hivyo, akitaka nidhamu, uwajibikaji na uzingatiaji wa taratibu za usalama viwe kipaumbele.

Mchengerwa ametoa maelekezo hayo ikiwa ni mwezi mmoja umepita tangu watumishi sita wa idara ya afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma, kufariki dunia baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupinduka katika ziwa Tanganyika, kutokana na mawimbi makali.

Tukio hilo lililotokea katika kijiji cha Kalalangabo, hata hivyo ilielezwa kuwa hawakuwa wamevalia koti la uokozi na taarifa zilieleza walikuwa zaidi ya wanane

Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa wakati akizungumza na Wananchi katika bandari ya Nyamisati kwa ajili ya makabidhiano ya boti za kutoa huduma ya afya.

“Ni muhimu kuhakikisha boti hizi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Kila safari izingatie usalama, ikiwemo kutobeba abiria zaidi ya wanane na kufuata ratiba rasmi za huduma za chanjo,” amesema.

Amesema uwekezaji huo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuhakikisha huduma za afya hazibaki kuwa za hiari, bali zinawafikia Watanzania wote kwa ubora na kwa wakati, bila kujali changamoto za miundombinu au jiografia.

Makabidhiano hayo yamefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Afya Kitaifa 2026 yanayofanyika Kibiti, yakilenga kuangazia mafanikio na changamoto katika sekta ya afya nchini.

Mchengerwa amesema boti hizo zitasaidia kutekeleza majukumu makuu manne, ikiwemo kupanua wigo wa kuwafikia walengwa, kuhakikisha upatikanaji wa chanjo kwa uhakika, kuimarisha usimamizi shirikishi wa huduma za afya na kuongeza uwezo wa utoaji huduma tembezi kwa wakati.

Ameeleza kuwa maeneo ya mwambao na visiwa yamekuwa yakikabiliwa na changamoto ya miundombinu, hali inayosababisha baadhi ya watoto kukosa chanjo kwa wakati na hivyo kuongeza hatari ya magonjwa yanayozuilika.

Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa wakati alipokuwa akiwasili katika bandari ya Nyamisati kwa ajili ya makabidhiano ya boti hizo

“Tunamlinda mtoto wa leo ili asiwe janga la kesho. Tukimuacha mtoto mmoja bila chanjo, tunaacha pengo katika ulinzi wa Taifa,” amesema.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Serikali, Grace Magembe, amesema boti hizo zitasaidia kufikia watoto ambao hawajapata hata dozi moja ya chanjo, ambao wengi wao wanapatikana katika maeneo ya mwambao na yasiyofikika kirahisi.

Amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika chanjo, ikifikia zaidi ya asilimia 90 ya utoaji wa chanjo kwa watoto, lakini bado kuna kundi ambalo halijafikiwa kikamilifu.

“Boti hizi zitaenda katika maeneo yenye changamoto kama Kibiti, Rufiji, Kigoma, Uvinza na Zanzibar. Lengo ni kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma,” amesema.

Aidha, amesema pamoja na utoaji wa chanjo, boti hizo pia zitatumika kutoa huduma nyingine za afya, ikiwemo elimu ya lishe na huduma mkoba kwa wananchi wa maeneo hayo.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF) nchini, Elke Wisch akizungumza katika hafla ya mabadhiano ya boti saba za huduma za chanjo

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF) nchini, Elke Wisch, ameipongeza Tanzania kwa mafanikio yake katika chanjo, akisema nchi imepunguza kwa kiasi kikubwa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo kwa watoto.

Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha watoto wote wanafikiwa.

“Tunapoadhimisha Wiki ya Afya, ni lazima tuhakikishe kila mtoto anayezaliwa Tanzania anapata chanjo zote muhimu za kuokoa maisha. Hakuna mtoto anayepaswa kuachwa nyuma,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mchengerwa amemwagiza Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia afya Ofisi ya Waziri Mkuu – Tamisemi, Profesa Mary Nagu kuhakikisha kituo cha afya Kibiti kinaboreshwa, huku akiagiza kutengwa kwa Sh500 milioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na kuboresha huduma.

Amesema kutokana na unyeti wa eneo hilo, ni muhimu wananchi wapate huduma karibu badala ya kusafiri umbali mrefu hadi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Baadhi ya wananchi wa Nyamisati wakiwa eneo la bandari ya Nyamisati kwa ajili ya makabidhiano ya boti hizo

Pia ameagiza halmashauri kuhakikisha zinaweka utaratibu maalumu wa ratiba za chanjo ili kufikia vijiji, visiwa na maeneo yote ya mwambao.

Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Joseph Kolombo, amesema wananchi wa eneo hilo wanaishukuru Serikali kwa uwekezaji huo, akibainisha kuwa bado wanakabiliwa na changamoto ya miundombinu ya barabara na uhaba wa magari ya huduma za afya.

Ameomba Serikali kuongeza msaada wa magari na gari la wagonjwai ili kuboresha usafirishaji wa wagonjwa na huduma za dharura.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibiti, Malela Toka, amesema wamechangia Sh250 milioni kwa ajili ya kukamilisha kituo cha afya Nyamisati, na wameiomba Serikali kukamilisha kiasi kilichobaki ili wananchi wapate huduma bora.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *