Dar es Salaam. Benki ya CRDB imeongoza kwa kupata faida kubwa kati ya benki zote za biashara nchini baada ya kupata faida ya Sh206 bilioni baada ya kodi katika robo ya kwanza mwaka huu.

Faida hiyo, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 18.9 ikilinganishwa na iliyopatikana katika kipindi kama hicho mwaka jana, imepatikana baada ya CRDB kufanya vyema katika viashiria vyote muhimu vinavyopima mwenendo wa utendaji wa taasisi za fedha, ikiwemo faida, ukubwa wa mali, amana za wateja na ufanisi wa uendeshaji.

Akizungumzia matokeo hayo bora zaidi katika historia yake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Abdulmajid Nsekela, amesema yanadhihirisha utekelezaji wa mkakati wa miaka mitano (Evolve Strategy 2023–2027).

“Tulilenga kupata mafanikio haya ndani ya miaka mitano na kweli, tukiwa katika mwaka wa tatu wa utekelezaji wa mkakati wetu wa miaka mitano, tumefanikiwa kuwa benki kubwa zaidi nchini na benki inayopata faida kubwa zaidi. Si bahati mbaya, bali ni utekelezaji wa mipango yetu ya ndani,” amesema Dk Nsekela.

Nsekela amesema matokeo hayo yanaonesha jinsi benki hiyo ilivyopiga hatua za ukuaji kwa kufanya vizuri katika viashiria vyote vya upimaji mwenendo bora wa kifedha, ikiwemo faida, jambo linaloifanya ikose mpinzani katika sekta ya benki nchini.

Akisisitiza kuhusu mkakati wake, Dk Nsekela amesema, wakiangalia wanakoelekea, anaiona Benki ya CRDB ikiimarisha zaidi uongozi wake sokoni kwa kuharakisha ukuaji katika sekta zenye mchango mkubwa kiuchumi, kupanua mfumo wake wa kidijitali na kutanua wigo wa huduma zake barani Afrika.

“Kwa sasa, hatupambanii kushika usukani wa soko, kwa kuwa tayari sisi ni viongozi. Kipaumbele chetu ni kujiimarisha hapa tulipo kwa kuendelea kubuni na kutoa thamani ya muda mrefu kwa wateja wetu, uchumi na wanahisa. Kwa sasa, Benki ya CRDB ndiyo kiongozi asiye na mpinzani sokoni,” amesema Dk Nsekela.

Mbali na faida sokoni, mali za benki hiyo zimeongezeka na kufika Sh23.9 trilioni, huku amana za wateja zikipanda kwa asilimia 9.0 hadi Sh16.3 trilioni, na mikopo iliyotolewa katika kipindi hicho ikifikia Sh14.7 trilioni, ikielekezwa zaidi katika sekta muhimu zinazochochea shughuli za kiuchumi.

Kadhalika, benki imeendelea na udhibiti wa vihatarishi, na uwiano wa mikopo chechefu umepungua hadi asilimia 2.85. Hali hii inaonesha ukuaji wa uwezo wa benki katika kutoa mikopo huku ikiimarisha mali zake, jambo linalosaidia kuifanya biashara hiyo ishamiri katika mazingira yote.

Kwa upande wa mapato, Benki ya CRDB imeendelea kufanya vizuri kwa kuwa na vyanzo mseto vya mapato, kwani yale yatokanayo na riba yaliongezeka hadi kufikia Sh388.8 bilioni, yakichochewa na ukuaji wa mikopo na ongezeko la mapato kutoka kwenye mali zinazozalisha riba.

Sambamba na hilo, benki imeendelea kuimarisha mapato yasiyotokana na riba, yakichangiwa na ongezeko la miamala kupitia huduma za kidijitali, huduma za benki kupitia mawakala na mifumo ya malipo.

Kadri wateja wanavyozidi kutumia huduma za kidijitali, Benki ya CRDB inaendelea kuongeza mapato yatokanayo na miamala huku ikiboresha uzoefu wa wateja, jambo linaloonesha nguvu ya mfumo wake wa kibiashara unaotegemea majukwaa ya kidijitali.

Licha ya kuendelea kuwekeza kimkakati katika teknolojia, ikiwemo maboresho ya mfumo mkuu wa uendeshaji pamoja na upanuzi wa shughuli zake kimataifa kupitia ufunguzi wa ofisi ya uwakilishi Dubai, CRDB imeendelea kudumisha nidhamu katika matumizi yake. Uwiano wa gharama za uendeshaji dhidi ya mapato ulibaki kuwa asilimia 41.6, ukionyesha uwezo wa benki hiyo kukua kwa ufanisi.

Kuhusu ufanisi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Profesa Neema Mori, amesema kuwa ufanisi ni nguzo muhimu na taasisi hiyo inatamani kuendelea kubaki kinara wa sekta ya benki nchini.

“Uongozi wetu haupimwi tu kwa ukuaji, bali kwa ufanisi wa ukuaji huo. Kuimarisha uwiano wa gharama za uendeshaji dhidi ya mapato wa asilimia 41.6 huku tukipanua shughuli zetu, kunaonesha uimara wa mfumo wetu wa uendeshaji. Tunaendelea kuhakikisha kuwa ukuaji wa mapato unatafsiriwa kuwa faida endelevu,” amesema Profesa Mori.

Profesa Mori amesema matokeo hayo pia yameleta tabasamu kwenye nyuso za wanahisa, ambapo faida inayotokana na uwekezaji wa mtaji wa wanahisa ilifikia asilimia 28.0, huku mtaji wa wanahisa ukiongezeka hadi kufikia Sh3.06 trilioni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *