Jake Sullivan, mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani katika serikali ya Joe Biden, ametoa taswira wadhiha na ya wazi ya sifa maalumu za mwenendo wa Iran katika mazungumzo ambayo inaweza kuwa ramani ya njia ya kuinasua serikali ya Marekani kwenye mkwamo ilionasa ndani yake hivi sasa. Sullivan ametoa taswira hiyo katika mahojiano na jarida la Foreign Affairs.
Katika anga tata ya mivutano mikali ya kidiplomasia iliyopo kati ya Marekani na Iran, wakati mwingine, chambuzi za maafisa wa zamani wa Marekani huwa zinazingatia zaidi uhalisia wa mambo kuliko ripoti yoyote rasmi. Alichoeleza Sullivan ni kutilia mkazo nukta ya msingi, kwamba Wairani “wanachukizwa na kitu chochote chenye ishara ya kuwataka wasalimu amri mbele ya vitisho na mashinikizo” na “wana ghera kubwa sana.”
Kwa mujibu wa mshauri huyo wa zamani wa usalama wa taifa wa Marekani, mistari myekundu ya Iran iko wazi kabisa; nayo ni kwamba, hawatakubali kamwe makubaliano yoyote yenye harufu ya kulazimishwa au kupiga magoti mbele ya ubabe na utumiaji mabavu. Maelezo hayo ni jibu la wazi kwa Trump na kwa kundi la wanamikakati wa Marekani ambao wangali wanaipigia upatu kaulimbiu ya kuipigisha magoti Iran kwa “mashinikizo ya juu kabisa.”
Sullivan ameashiria mtindo wa ufanyaji mazungumzo anaotumia Rais wa Marekani na kubainisha kwamba, Trump anapendelea makubaliano ambayo ataweza kudai kuwa yamefikiwa kwa “kuulazimisha” upande wa pili, katika hali ambayo Iran haitaukubali katu utaratibu utakaoashiria kuwa wao wamelazimishwa au wameshindwa; na mgongano huo wa kimiamala ndio unaofanya iwe ni vigumu kufikia makubaliano yoyote ya kudumu.
Sullivan sio sauti pekee inayokosoa sera za mashinikizo ya juu kabisa za Trump. Hata miongoni mwa maafisa wa sasa na wa zamani wa bunge la Marekani, pamoja na wachambuzi waandamizi wa nchi hiyo, kuna kundi kubwa la wataalamu ambao, sambamba na kukosoa waziwazi muelekeo wa Trump, wamesisitiza juu ya ulazima wa kuachana na madai ya kutimiziwa matakwa ya kiwango cha juu kabisa, na badala yake, kuheshimu mistari myekundu ya Iran. Seneta Chris Murphy, Mdemokrati mwenye ushawishi na mjumbe wa Kamati ya Uhusiano wa Nje ya Seneti ya Marekani ameonya kwa kauli iliyo wazi, kwamba kung’ang’ania matakwa ya kiwango cha juu kabisa kwa kufuata muelekeo wa Trump kutafuta hadi kiwango cha sifuri uwezekano wa kufikiwa makubaliano yoyote ya nyuklia; na akasisitiza kwamba, njia pekee inayoendana na uhalisia, ni kurejea kwenye msingi wa JCPOA na kisha kujitahidi kufikia makubaliano imara zaidi, na si kulazimisha masharti yasiyowezekana, kama kutaka kusimamishwa moja kwa moja urutubishaji urani au kufumuliwa kikamilifu mpango wa makombora wa Iran.
Robert Malley, mjumbe mwandamizi wa timu ya zamani ya Marekani katika mapatano ya nyuklia ya mwaka 2015 na mmoja wa maafisa wakuu wa serikali ya Biden, naye pia amekosoa katika chambuzi zake kadhaa muelekeo anaofuata Trump na akauelezea kama ifuatavyo mgongano mkubwa uliopo kati ya mtindo wa mazungumzo anaotumia rais huyo wa Marekani na muundo wa uchukuaji maamuzi uliopo nchini Iran: Trump anataka apate matokeo mengi na kwa haraka, anataka kujionyesha pia kwa ushindi anaopata, lakini uongozi wa Iran unafuatilia mbinu ya “mchezo wa muda mrefu” na uko tayari kuhimili gharama kubwa na za muda mrefu kwa sababu ya kutolegeza msimamo katika maslahi yake ya msingi, kwa sababu katika utamaduni wa kisiasa na wa kimkakati wa Iran, kujenga taswira ya “kulegeza msimamo mbele ya mashinikizo” ni jambo lisilokubalika.
Malley, ambaye kwa miaka kadhaa amekaa kwenye meza ya majadiliano na timu ya mazungumzo ya Iran, amewahi kueleza mara nyingi kwamba, kuelewa “ghera ya kitaifa” na “kuchukizwa na udhalilishaji” ni kitu muhimu kwa mwanadiplomasia yeyote, na kwamba, kwa sera yake ya “mashinikizo ya juu kabisa” na kuropoka maneno ya utoaji vitisho, Trump amejenga mazingira yaleyale ya udhalilishaji ambayo Wairani hawajawahi kuwa na wala hawatokuwa tayari katu kufanyia mazungumzo.
Nate Swanson, mkurugenzi wa zamani wa faili la Iran katika Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani na mchambuzi mashuhuri katika Tanuri Fikra la Atlantiki, yeye pia amekosoa mtazamo huo wa Trump na kueleza kwamba sera ya “mashinikizo ya juu kabisa” hadi sasa imeshindwa kuleta mabadiliko ya msingi katika maamuzi ya Iran; na kinyume chake, imeipa funzo Tehran la namna ya kuzima mashinikizo hayo kwa kutumia mbinu ya Uchumi wa Muqawama na kuwa na mchanganyiko wa washirika wa kibiashara.
Katika sehemu nyingine ya mahojiano yake na Jarida la Foreign Affair, Jake Sullivan ameashiria pia mabadiliko ya kimkakati yaliyojiri katika eneo ambayo hayajazungumziwa kwa namna inayostahiki: ambayo ni kubadilika kitisho cha kinadharia cha Iran cha kuufunga Mlango-Bahari wa Hormuz na kuwa “uwezo wa kivitendo.”
Kwa mujibu wa Sullivan, mabadiliko hayo ya kwenye medani yamepangua milingano ya nguvu za kuzuia hujuma na kukifanya kitisho ilichotoa Iran kiwe ” cha kuaminika zaidi”. Afisa huyo mwandamizi wa serikali ya Biden anatabiri kuwa, katika siku za usoni, Tehran itatekeleza operesheni kubwa zaidi za kudhibiti kivuko hicho muhimu cha baharini, na huo utakuwa moja ya uhalisia mpya katika eneo.
Maelezo hayo ya Sullivan yanafikisha ujumbe wenye hali mbili kwa wapangaji sera wa Washington: wa kwanza ni kwamba, mashinikizo ya juu kabisa sio tu hayajaipigisha magoti Iran na kuifanya isalimu amri, lakini pia yameongeza uwezo wake wa uchukuaji hatua za kwenye medani. Na pili ni kuwa, kosa lolote la kimahesabu litakalofanywa katika mazungumzo linaweza kuubebesha gharama kubwa usalama wa nishati duniani.
Kwa maneno mengine, Sullivan na maafisa wenzake wa serikali ya Biden wamefikia hatua ya kuelewa kwamba kuzungumza na Iran kwa kutegemea “msimamo wa nguvu” hakumaanishi tena kuwa na uwezo wa kutoa masharti ya upande mmoja, bali kunahitaji kuelewa kiuhalisia mistari myekundu ya upande wa Iran na uwezo wake kivitendo. Huenda matunda muhimu zaidi ya uchambuzi huo, yakawa ni kubaini kufikia tamati zama za “kupigishwa magoti” mbele ya mashinikizo; na kuanza zama mpya ambapo Washington, itakuwa haina budi isipokuwa kuheshimu ghera ya kitaifa ya Iran na uwezo wake wa kwenye medani…/