Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada ya Dharura kwa Watoto, UNICEF, limetangaza kuwa watoto 43,000 wameuawa au kujeruhiwa tangu kuanza kwa vita nchini Sudan.

Kwa mujibu wa taarifa, Umoja wa Mataifa umerekodi zaidi ya matukio 5,700 ya ukiukaji mkubwa dhidi ya watoto kote Sudan vita vya sasa vya ndani vianze Aprili 2023.

Matukio haya yameathiri angalau watoto 5,100, na kusababisha vifo au ulemavu kwa watoto 4,300.

Ripoti mpya ya UNICEF iliyopewa jina “Darfur: Miaka 20 ya Watoto Katika Hatari” inaonyesha kuwa katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ya mwaka 2026 pekee, angalau watoto 160 waliuawa na wengine 85 wakajeruhiwa.

Tangu Aprili 2024, zaidi ya ukiukaji 1,500 wa haki za watoto umeripotiwa katika eneo la Al-Fashir ambalo lilitekwa na waasi wa RSF, na matukio hayo yamesababisha vifo au ulemavu wa zaidi ya watoto 1,300.

UNICEF imebaini kuwa ukiukaji huo unahusisha unyanyasaji wa kingono, kuingizwa kwa watoto katika makundi yenye silaha, pamoja na madhara yatokanayo na vilipuzi na matumizi ya ndege zisizo na rubani.

Awamu mpya ya vita vya ndani nchini Sudan ilianza tarehe 15 Aprili 2023, baada ya mvutano kati ya jeshi la kitaifa linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye ni rais wa mpito wa Sudan na wanamgambo wa RSF wanaoongozwa na Mohamed Hamdan Dagalo (Hemedti). Serikali ya Sudan imewaorodehsa wanamgambo hao watenda jina kama kundi la kigaidi. Aidha serikali ya Sudan inautuhumu utawala wa Umoja wa Falme za Kiarabu kuwa unawuanga mkono magaidi hao wa RSF ambao wanatekeleza mauaji ya kimbari hasa katika eneo la Darfur.

Juhudi mbalimbali za upatanishi wa kimataifa hadi sasa hazijafanikiwa kukomesha mapigano hayo.

Mgogoro huo umeacha maelfu ya watu wakiwa wamepoteza maisha, karibu watu milioni 13 wakikimbia makazi yao, na sehemu kadhaa za nchi zikiwa katika hatari ya njaa.

Sudan, tangu kupata uhuru mwaka 1956, imepitia kipindi kirefu cha misukosuko na machafuko, ikiwa ni pamoja na majaribio 20 ya mapinduzi na vita viwili vikubwa vya wenyewe kwa wenyewe kati ya 1955–1972 na 1983–2005, ambavyo hatimaye vilisababisha kujitenga kwa Sudan Kusini mwaka 2011.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *