
Katikati ya mambo mengi yanayojiri ndani na nje ya nchi, lipo jambo linalopaswa kujifunza, hasa katika kipindi ambacho ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 ipo wazi na mijadala inaendelea. Tafakuri kuhusu Iran yenye vikwazo kwa miaka 47, lakini inaweza kuitetemesha dola ya Marekani ambayo ndiyo hujinasibu kama “the superpower”, yaani ina nguvu zisizomithilika.
Mafundisho ya vitabuni, mtoto mdogo Daud kumpiga na kumuua pandikizi la mtu, Goliati, ni darasa kuwa ‘miguvu’ bila akili ni hasara. Daud kwa kutumia kombeo, na kupawa chake cha ulengaji shabaha, jumlisha ujasiri wa asili aliokuwa nao, aliweza kumtuliza Goliati, mbabe wa mapigano ya vita aliyekuwa ameshindikana.
Inafanana na simulizi ya Biblia, kitabu cha Waamuzi 4 na 5, kamanda wa jeshi la Kanani, Sisera, aliyeogopwa, na aliyewatesa wana wa Israel kwa miaka 20, aliuawa na mwanamke, Jael, mke wa Heberi (Heber the Kenite). Ni kwa sababu Jael alitumia akili na maarifa. Na aliyeongoza jeshi la Israel lililouangusha utawala wa Kanani ni mwanamke, Deborah.
Wosia wa aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Iran (Rahbar-e Moazzam), Ayatollah Ali Khamenei, kwa Wairan, katika siku za mwisho za uhai wake ulihusu umoja kama silaha kuu ya kushinda udhalimu na uvamizi. Aliwataka kutoogopa vitisho vya Rais wa Marekani, Donald Trump, aliyetamba kuwa nchi yake ndiyo yenye jeshi lenye nguvu kuliko mataifa yote ulimwenguni. Khamenei alisema “mwenye nguvu hutokea kupigwa na dhaifu.”
Kinachoendelea Mashariki ya Kati, mtikisiko wa dunia, mateso ya gharama za maisha kupanda, sababu ikiwa Iran kuushikilia mlango bahari wa Hormuz, inakupa picha ileile ya Daud dhidi ya Goliati kwa kombeo, Jael alivyomuua Sisera kwa kutumia kigingi cha hema na nyundo, au Deborah kwa maarifa na wito wa hali ya juu, alivyowezesha anguko la Kanani.
Pamoja na kila sifa ambayo Iran inaweza kupewa, lakini siri ipo kwenye umoja na mshikamano. Kama nchi walikuwa na tofauti zao za ndani kisiasa. Maandamano ya kudai haki yalijiri. Baada ya uvamizi wa Marekani na Israel, vilevile kuuawa kwa Ayatollah Khamenei, haraka sana Wairan waliungana kwa ajili ya kuilinda nchi yao. Hata vikundi vya uasi vilijisalimisha jeshini, na kuomba kupangiwa majukumu ya kivita ili kuwakabili Wamarekani na Waisrael. Ni mshikamano wa ndani uliowezesha China kuipiga Japan katika vita ya Sino-Japanese II. Wachina ilibidi waungane na waache kupigana wao kwa wao, kwa maslahi ya taifa lao. Japan waliwavizia Wachina walipokuwa kwenye mapigano ya ndani, wakawavamia. Haraka sana, Wachina walisitisha vita ya ndani na kuungana kupigana na Wajapan. Kisha, baada ya kumalizana na Japan, Wachina walirudi tena kupigana wenyewe kwa wenyewe.
Kulikuwa na mchuano mkali wa kugombea madaraka kati ya Chama cha Kuomintang (KMT) ambacho kilikuwa kinawakilisha daraja la watawala na matajiri China dhidi ya Chinese Communist Party (CCP), kilichowakilisha watawaliwa, hasa makabwela.
Kuomintang na Communist, walipigana vita ya wenyewe kwa wenyewe. Ilianza Agosti mosi, 1927 lakini pande zote mbili zilikubaliana kusitisha mapigano kisha kuunganisha nguvu dhidi ya Japan katika Vita ya Sino-Japanese II kati ya mwaka 1937 mpaka 1945, ikikutana juu kwa juu na Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Baada ya vita ya Sino-Japanese pamoja na vita Kuu ya Pili ya Dunia kwisha, Kuomintang na Communist walitengana na kuchapana wao kwa wao mpaka Mei mosi, 1950, Communist waliposhinda na kushika hatamu ya kuongoza Jamhuri ya Watu wa China.
Swali, Tanzania inapopata adui wa nje, Watanzania wataungana au itakuwa fahari kwa upande mmoja? Haitakuwa furaha kwa watakaoona wamepata mshirika kutoka nje? Inakumbusha nyakati baada ya machafuko ya Oktoba 29, 2025, kuna watu waliomba Trump aivamie Tanzania, kisha achukue madini, halafu baada ya utawala uliopo kuanguka, eti nchi tungeanza upya. Ni mawazo ya Watanzania dhidi ya Tanzania.
Hata sasa, baada ya mwenyekiti wa tume hiyo, Mohamed Chande Othman kusoma ripoti, badala ya kutafakari na kutafuta majibu ni kwa namna gani nchi inaweza kutoka ilipo kwenda mbele, ikiwa na umoja wa kitaifa, kinachotokea sasa ni mabishano. Swali ni moja, mabishano yana shabaha ya aina gani? Tume imesema idadi ya waliopoteza maisha katika ghasia za Oktoba 29 ni 518. Hawa ni watu wengi. Kama taifa ilitakiwa kutuliza kichwa na kujiuliza; Inakuwaje ilishindikana kupata dirisha la mazungumzo, matokeo yake Watanzania 518 walipoteza maisha? Swali hilo linaweza kusogeza hali ya majuto kwa kila upande kwa kufunga milango yote ya majadiliano na mwafaka. Jitihada zote za kufungua japo dirisha, ziligonga ukuta.
Yaliyotokea yanapaswa kumsikitisha kila mtu. Pande zote zinastahili lawama. Waliotumia nguvu kudhibiti ghasia, na waliochochea machafuko. Hakuna aliyekuwa hajui vurugu zingeibuka kuna mambo yangetokea, vifo, majeruhi na uharibifu wa mali. Binafsi kwa kutambua hayo, ndiyo maana kupitia safu hii, katika gazeti letu hili la Mwananchi, niliandika mfululizo makala za kuomba nusura ili ghasia zisitokee.
Ushuhuda wa ghasia za Oktoba 29 una mnyororo mrefu. Kuna waliopoteza maisha katika makabailiano, wengine walifia nyumbani kwa kushindwa kupata matibabu. Wapo wafanyabiashara waliuvaa umaskini kwa kuwa biashara zao ziliharibiwa, wengine zilivunda. Mathalan, wafanyabiashara ya vitoweo ambao mali zao zilioza. Maumivu hayamithiliki kwa waliopoteza ajira, kisa waajiri wao kupata hasara.
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alisema maadui wa nchi ni watatu; ujinga, maradhi na umaskini. Mivutano ya sasa inaonesha kuwa nchi ina adui wa nne, ambaye ni migawanyiko na kufikiri kuna watu nje watasaidia kurekebisha ndani kwao. Ripoti ya Jaji Chande badala ya kuwaunganisha Watanzania, inaleta mabishano ambayo hayana tija. Taifa linahitaji mshikamano.