Dodoma. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema jamii imeweka mkazo mkubwa katika taaluma, huku ikisahau malezi ya msingi ya kuwajenga watoto kuwa wazazi bora wa baadaye.

Aidha, amesema viongozi wa dini wamerudi nyuma katika mapambano ya rushwa, badala yake wamegeukia kwenye mapambano ya kisiasa.

Waziri Makonda amesema hata maadili shuleni hayafundishwi, jambo alilohoji kama viongozi hao wanaona raha kuongoza watu wa aina hiyo, wala rushwa na watumiaji wa dawa za kulevya kwa siku za usoni.

Ametoa kauli hiyo leo, Jumatano, Aprili 29, 2026, katika hafla ya uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mmomonyoko wa Maadili 2026/27 hadi 2036/37 jijini Dodoma.

Makonda amesema mkakati huo unatekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa mwaka 2024, akitaka kuwepo mfumo wa pamoja unaounganisha Serikali, familia na wadau wengine kulinda maadili na utambulisho wa Taifa.

Amesema kuyumba kwa familia ndicho chanzo kikuu cha changamoto nyingi za kijamii zinazoonekana sasa.

“Familia ikiyumba ni sawa na msingi wa Taifa uliobomoka. Bila familia bora na imara, Taifa halipo,” amesema.

Makonda ameeleza mwelekeo wa malezi ya sasa, akisema jamii imejikita zaidi katika kuwaandaa watoto kufanikiwa kitaaluma, lakini si kuwaandaa kuwa wazazi bora.

“Leo tunawaandaa watoto kuwa madaktari, wanasheria na wahasibu, lakini hatuwaandai kuwa baba au mama bora. Matokeo yake wanalelewa na mitandao ya kijamii,” amesema.

Amesema hali hiyo imechangia kuongezeka kwa familia zisizo imara, idadi kubwa ya kinamama wanaolea watoto peke yao (single mothers), pamoja na watoto wenye hasira na chuki dhidi ya wazazi wao.

Waziri huyo amesema kwa sasa hakuna ujumbe unaotolewa na viongozi wa dini katika siku za hivi karibuni kuhusu kukemea rushwa na dawa za kulevya, ambao walikuwa wakizifanya miaka 15 iliyopita.

Amesisitiza kuwa lawama nyingi ambazo viongozi wa dini wanazitoa, wanasahau zinatoka kwa waumini wao, ikiwemo rushwa, dawa ya kulevya na mambo mengi yasiyo na staha yanatendwa na waumini wanaotoa sadaka kwenye nyumba za ibada.

“Tutengeneze kizazi kizuri cha kubanana na waumini. Nilipokuwa mkuu wa mkoa wa Arusha nilifanya uchunguzi nikagundua, walimu wa shule za msingi na sekondari licha ya kuwepo kwa vipindi vya dini, lakini hakuna wanaokwenda kufundisha, na sababu ni kwamba watoto wale hawana sadaka,” amesema Makonda.

Kwa upande wa viongozi, ametaja alichokiita ni uoga, kwamba viongozi wengi wamekuwa waoga na wenye ndoto ya kutaka kupendwa, wakihofia kupoteza kura zao.

“Taifa linaponzwa na uoga. Tuna viongozi waoga na ndoto ya kutaka kupendwa-pendwa. Hata palipo na mambo ya msingi mnahisi mkisema ukweli mtaharibu kura zenu. Hii kasumba imeenda mbali zaidi,” amesema Makonda.

Amesema watu wengi kabla hawajaingia madarakani huwa wanapiga kelele za rushwa, lakini wakiingia madarakani hukaa kimya, na sababu ni njaa na wakati mwingine misingi ya familia kuwa wameiacha.

Ametolea mfano kuwa alipokuwa kwenye mkutano wa Bunge la Katiba, alishuhudia watu wakilalamika na kukemea rushwa, lakini baada ya kupata madaraka walikaa kimya, akisema baadhi yao hawakuwa na malezi ya kifamilia na walikosa malezi ya dini.

“Kuna wangapi mliwasikia wakikemea rushwa kabla ya kupata madaraka, lakini walipoingia jikoni wakakaa kimya. Tuliwaacha kwenye misingi ya mafundisho ya dini. Tusihangaike na matawi wala kuilaumu Serikali pekee, twendeni tupambane kwa pamoja,” amesema.

Amesema Watanzania wanapaswa kukubali kutengeneza kizazi chenye misingi na utu katika kuitazama Tanzania ya kesho, huku akisisitiza kila mzazi kumsimamia mwanawe katika maadili ili awe baba au mama bora wa kesho, badala ya kumwandaa kuwa daktari au mwenye vyeo vingine pekee.

Kwa upande wake, amesema hana shida kwa sababu hafikii kugombea cheo chochote, bali anachowaza ni kuchapa kazi atakazokuwa amekabidhiwa, hivyo ataendelea kuwa muwazi na mkweli, na hataona aibu kukemea rushwa, dawa za kulevya na mambo mengine.

Kuhusu wanahabari, amewaagiza kutanguliza uzalendo mbele na kuliona Taifa kwanza, lakini kila wanachotuma wafikiri kama kitakuwa na faida gani kwa nchi yao, kuliko kukimbilia mambo yasiyo na maudhui ikiwemo umbea na watu waliofumaniana.

Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Doroth Gwajima, amesema Serikali kupitia wizara hizo mbili imejipanga kuhakikisha Taifa linakuwa na utoshelevu wa kimaadili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *